Bunge la Marekani laidhinisha fedha kwa Afghanistan
28 Julai 2010Idhini hiyo imetolewa wakati ambapo kiongozi huyo wa Marekani anaandamwa na kashfa ya hati za siri za kijeshi zilizovuja kadhalika upinzani kutoka kwa wanasiasa wa chama chake cha Demokratik.Wanasiasa wengi wa chama cha Republik ndio waliouidhinisha mswada huo.Baraza la Senate lilishatoa ridhaa yake na anasubiriwa Rais Obama kuutia saini.Bunge hilo la Marekani lililo na wanasiasa wengi wa Chama cha Rais Obama cha Demokratik limeuidhinisha mswada huo baada ya kusuasua kwa kipindi cha miezi sita.Baraza la wawakilishi liliudhinisha mswada huo kwa kura 308 na kupingwa kwa 114.Mswada huo utakiruhusu kiasi cha dola bilioni 37 kutumiwa kupambana na wapiganaji wa Taleban nchini Afghanistan.Ifahamike kuwa wengi ya waliouidhinisha mswada huo ni wanasiasa wa Republik na wala sio wa chama chake cha Demokratik.Jumla ya wanasiasa 102 waliupinga mswada huo.Baraza la Senate tayari lilishauidhinisha mswada huo unaosubiri kutiwa saini na Rais Obama.
Republik mstari wa mbele
Mswada huo umezua mgongano mkubwa kati ya wanasiasa wa Demokratik.Kwa upande wake Wizara ya Ulinzi ya Marekani ,Pentagon ilitumia mbinu zote kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapatikana na ikajitetea kuwa endapo hilo halingefanyika ifikapo mwezi wa Agosti,ingelazimika kuipunguza mishahara ya wafanyakazi wa kawaida ili kuliziba pengo hilo. Wanasiasa wanaouunga mkono mswada huo walisisitiza kuwa si sahihi kuzichelewesha fedha zitakazotumiwa kuyafadhili mahitaji ya wanajeshi ambao tayari wameshapelekwa vitani.
Chini ya mpango huo mpya wa dharura,Rais Obama ataweza kuyafadhili mahitaji ya kupeleka Afghanistan wanajeshi alfu 30 wa ziada vilevile baadhi ya operesheni za Iraq.Kiasi hicho cha dola bilioni 37 ni nyongeza ya dola bilioni 130 ambazo tayari zimeshaidhinishwa na Bunge la Marekani mahsusi kwa shughuli hiyo kwa mwaka huu.Kiasi cha dola trilioni 1 kimeshatumiwa kuzifadhili operesheni za Afghanistan na Iraq tangu mwaka 2001.
Kashfa ya Wiki-leaks
Yote hayo yanatokea wakati ambapo Marekani inaandamwa na kashfa ya hati za siri za kijeshi zilizovuja.Nyaraka hizo zilichapishwa kwenye mtandao unaofichua taarifa za siri wa Wikileaks,na zinadai kuwa wanajeshi wa Marekani walizificha taarifa za vifo vya raia wa kawaida na kwamba Pakistan inawaunga mkono wapiganaji wa Taleban ila bado inaendelea kupokea misaada kutoka kwa Marekani.Hata hivyo Rais Obama aliusisitizia umuhimu wa kuendelea na mkakati huo hata baada ya kuvuja huko.Badala yake Rais Obama alifafanua kuwa hakuna jipya lililojitokeza kwenye taarifa hizo.Kamanda mkuu mteule wa jeshi la Marekani,Jenerali James Mattis aliziafiki kauli hizo.
Kulingana na wachambuzi,hali yote kwa jumla inatoa picha tofauti kwani kwa upande mmoja serikali inataka kuungwa na mkono na umma katika hivyo na kwa upande wa pili inajiandaa kuviondoa vikosi vyake ifikapo mwezi wa Julai mwakani kama alivyotangaza Rais Obama.Baadaye hii leo mjumbe maalum wa Marekani Richard Holbrooke atarakiwa kujibu maswali mbele ya jopo maalum la bunge kuhusu makakati huo wa Afghanistan.
Kwa upande mwengine,serikali ya Afghanistan inayotaka kuisimamia misaada yake ya kigeni,imeeleza kuwa Marekani imeshindwa kupambana na wanaowaunga mkono wapiganaji wa Taleban wanaoripotiwa kujificha Pakistan.
Ngoma ya kulaumiana
Pakistan kwa upande wake imeyakanusha madai hayo ijapokuwa ina uhusiano wa muda mrefu kati ya vitengo vyake vya ujasusi na jeshi na kundi la Taleban.
Vifo vya raia wa kawaida vilivyosababishwa na wanajeshi wa kigeni ni jambo linalozua mivutano mikali kati ya Rais wa Afghanistan Hamid Karzai na viongozi wa mataifa ya magharibi wanaomuunga mkono.Kiasi cha wanajeshi laki moja na nusu wanashiriki katika mapambano hayo dhidi ya waasi.
Mwandishi:Mwadzaya Thelma-RTRE
Mhariri:Mtullya Abdu/