Bunge la Marekani lachunguza udukuzi dhidi ya Urusi
5 Januari 2017Kikao cha mahojiano cha kamati ya huduma za majeshi ya taifa kuhusu kitisho mtandaoni leo Alhamis kinakuja siku moja kabla ya rais mteule wa Marekani Donald Trump akitarajiwa kupewa taarifa na wakurugenzi wa mashirika ya ujasusi CIA na lile la uchunguzi wa makosa ya jinai FBI, pamoja na mkurugenzi wa usalama wa taifa, kuhusiana na uchunguzi juu ya madai ya udukuzi uliofanywa na Urusi.
Trump amekuwa akikosoa sana ugunduzi wao, hata kuonekana kuunga mkono mtazamo wa mwanzilishi wa tovuti inayofichua masuala ya siri za serikali Julian Assange kwamba Urusi haikumpa barua pepe za chama cha Democratic zilizodukuliwa.
Lakini msemaji wa Ikulu ya Marekani ya White House, Josh Earnest amesema tathmini iliyotolewa kwa pamoja na vyombo vya upelelezi inaonesha wazi kuwa Urusi ilikuwa ikiingilia shughuli za uchaguzi nchini Marekani.
"Tarifa hiyo ambayo ilitolewa na vyombo vya upelelezi Oktoba mwaka 2016 kabla ya uchaguzi inaweka wazi kwamba Urusi ilikuwa inaingilia kati katika uchaguzi wetu na kuwalikisha mtazamo wa pamoja wa mashirika 17 tofauti ya upelelezi. Hii si kawaida ya vyombo hivi kufanya kazi. Hali ya mawazo yanayolingana, hususan hali ikiwa ya mvutano, ni suala la kutafakari. Uamuzi wa vyombo vya upelelezi, sio tu kufikia hitimisho lakini kuiweka wazi ripoti yao, ni jambo kubwa na nafikiri inaakisi kina cha hali yao ya kuamini tathmini yao."
Kujitayarisha kwa mashambulizi yajayo
Kikao hicho cha kamati ni cha kwanza katika mfululizo wenye lengo la kufanya uchunguzi juu ya kile kinachofikiriwa kuwa ni mashambulizi ya mtandaoni yaliyofanywa na Urusi dhidi ya maslahi ya Marekani na kutengeneza ulinzi imara wa kutosha kuhusu uingiliaji katika siku zijazo.
Shutuma za Urusi kuingilia katika uchaguzi wa mwaka 2016 kwa kudukua kurasa za barua pepe za chama cha Democratic zimeizunguka serikali mjini Washington kwa wiki kadhaa. Rais Barack Obama alilipiza kwa Urusi mwishoni mwa mwezi Desemba kwa kuchukua hatua ya kuweka vikwazo vinavyolenga mashirika ya ujasusi ya Urusi, lile la GRU na FSB, ambayo Marekani ilisema yanahusika. GRU ni shirika la Urusi linaloshughulika na masuala ya ujasusi wa kijeshi. Lile la FSB ni mrithi wa shirika la wakati wa enzi za Umoja wa Kisovieti la KGB.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Grace Patricia Kabogo