1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Irak lakutana kwa dharura

Oummilkheir13 Aprili 2007

Wairak wamedhamiria kutia njiani utaratibu wa kisiasa

https://p.dw.com/p/CHGJ
Picha: picture-alliance/dpa

Kikao hicho cha dharura kilichoitishwa kama ishara ya “kutojali vitishso vya magaidi” kimeshafunguliwa katika jengo hilo hilo la bunge mjini Baghdad ambako jana mtu aliyeyatolea mhanga maisha yake alijiripua na kuwaangamizia maisha watu wengine wanane.

Wabunge wachache tuu lakini ndio wanaohudhuria mkutano huo ulioanza kwa kusomwa Qoraani na kufuatiwa na hotuba ya spika wa bunge Mahmoud MACHHADANI.Wengine zaidi ya 40 wamekwama nje kutokana na hatua kali za usalama.

“Kikao hiki ni onyo bayana kwa magaidi na wote wale wanaotaka kujaribu kuuzuwias utaratibu wa kisiasa ambao tumejitolea kuukamilisha”Amesema Mahmoud Machhandani ambae ni wa madhehebu ya sunni.

Watumishi watatu wa mkahawa wa bunge wamekamatwa na wanahojiwa na polisi kuhusiana na mashambulio hayo ya jana.Mbunge wa kishiya Hassan al Senaid anasema hata hivyo hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa dhidi yao.

“Uchunguzi unaendelea bungeni,hadi wakati huu watumishi watatu wamekamatwa” ame´sema hayo Hassan el Sanaid mbele ya waandishi habari hii leo.

Shambulio dhidi ya bunge la Iraq limelaaniwa kote ulimwenguni.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema:

“Nimeingiwa kwa mara nyengine tena na wasi wasi mkubwa kutokana na matumizi ya nguvu yasiyokwisha na hasa kutokana na shambulio lililofanywa safari hii bungeni.Visa kama hivi vya matumizi ya nguvu,haviwezi hata kidogo kuhalalika,mamoja vimesababishwa na nini.”

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amewatolea mwito viongozi wote wa Irak waungane ili kumaliza matumizi ya nguvu na kujenga nchi ambako watu wataishi kwa amani na utulivu.

Muakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya Javier Solana amelaani “shambulio hilo la kigaidi” lililogharimu maisha ya watu wanane.Ametuma risala za rambi rambi kwa familia za wahanga na serikali ya Irak.Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Ulaya amesema tunanukuu: “shambulio la kigaidi dhidi ya wakala wa mamlaka ya umma wa Irak ni ushahidi unaoonyesha kwa mara nyengine tena,kila la kufanywa lifanywe kusitisha matumizi ya nguvu yanayowasababishia machungu wananchi wa Irak.”Mwisho wa kumnukuu muakilishi wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya Javier Solana.

Shambulio la jana bungeni limejiri saa chache tuu baada ya shambulio kama hilo dhidi ya daraja ya mjini Baghdad ambapo watu kumi walipoteza maisha yao.Na yote hayo yanatokea licha ya hatua kali za kuimarisha usalama zilizoanzishwa tangu miezi miwili iliyopita na vikosi vya Marekani na vile vya Irak mjini Baghdad.