Bunge la Ethiopia laridhia sheria, kuwekea vikwazo mashirika ya kiraia yanayofadhiliwa zaidi.
7 Januari 2009Chini ya sheria hiyo, Shirika lolote litakalokuwa linapokea ufadhili wa zaidi ya asilimia 10, kutoka nje, litachukuliwa kuwa ni Shirika la Kigeni na hivyo kupigwa marufuku kuendesha shughuli zozote za kijamii, jinsia, haki za watoto na kutatua mizozo katika eneo hilo.
Aidha upinzani hawakupigia kura muswada huo, ulioidhinishwa, baada ya kupigiwa kura 327 dhidi ya 79.
Mbunge wa upinzani nchini humoTemesgen Zewdie amesema muswada huo ni jaribio la chama tawala kupiga marufuku vyote vinavyoonekana kutishia nafasi yake hiyo.
Kiongozi mwingine wa upinzani Beyenne Petros amesema ni jambo baya kwao kuona muswada aliouita kuwa ni wa kikatili ukipitishwa, kutokana na kwamba serikali ya nchi hiyo haitaki kuona mashirika ya kijamii yanayojitolea yakitekeleza majukumu yake, ajenda ikiwa ni kufunika mwenendo wake, ambao ni kusaidia jamii.
Lakini hata hivyo serikali ya nchi hiyo imesisitiza kwamba sheria hiyo haikutungwa kuzuia shughuli za mashirika hayo yasiyo ya kiserikali, bali ni kwa ajili ya kulinda usalama na matakwa ya raia.
Kiongozi wa serikali katika bunge la nchi hiyo, Hailemariam Desalegn amesema Mashirika ya Kiraia nchini humo yatakuwa na uwezo wa kufanya kazi zao bila ya kizuizi chochote, iwapo yataheshimu sheria za nchi hiyo.
Marekani na Uingereza nchi ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa misaada katika taifa hilo la pembe ya Afrika, zimeelezea kutoridhishwa kwao na sheria hiyo.
Nalo Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limekosoa sheria hiyo kwa kusema kuwa inavunja haki za binadamu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kijerumani linalopambana na Njaa, lenye makazi yake mjini Addis Ababa, Bernhard Meier amesema kwa mtazamo wao, wanaona kuwa sheria hiyo ina matatizo.
Serikali ya Ethiopia imesisitiza kuwa ushirikiano wake na nchi za magharibi, utabakia palepale, licha ya kupitishwa kwa sheria hiyo.
Ethiopia, ambayo inatarajia kufanya uchaguzi wake mwaka 2010 ni moja ya nchi duniani, ambazo zinapokea misaada kwa wingi.