1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge kuchunguza madai ya Trump dhidi ya Obama

6 Machi 2017

Mwenyekiti wa Republican wa kamati teule ya ujasusi bungeni Devin Nunes, amesema kamati yake itayashughulikia madai ya Trump, hasa baada ya ikulu ya Marekani kuliomba bunge kuyachunguza madai hayo.

https://p.dw.com/p/2Yh0I
USA Trump Rede vor dem Kongress
Picha: Reuters/J. Lo Scalzo

Mkurugenzi wa shirika la upelelezi wa ndani nchini Marekani FBI James Comey ameitaka idara ya uchunguzi kuyakana hadharani madai ya Rais Donald Trump kwamba raisaliyemaliza muda wake Barrack Obama alidukua mawasiliano yake ya simu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka uliopita.

Likiwanukuu maafisa wakuu wa Marekani, gazeti la New York Times limeripoti kuwa mkurugenzi huyo wa shirika la upelelezi wa ndani  FBI James Comey anaamini  madai ya Trump yasiyokuwa na msingi wowote dhidi ya mtangulizi wake ni uwongo. Hadi sasa idara hiyo ya upelelezi haijatoa tamko rasmi kuhusiana na madai ya Trump. Kulingana na gazeti hilo, Comey alitoa ombi hilo kwa sababu hakuna ushahidi wa kuyathibitisha madai hayo kando na kwamba yanaashiria kuwa FBI ilivunja sheria.

Aliyesimamia idara ya ujasusi ayakana madai

Akihojiwa na runinga ya NBC, mkurugenzi wa idara ya ujasusi nchini Marekani James Clapper aliyesimamia mambo ya ujasusi wakati Obama alipokuwa madarakani amekanusha kudukuliwa kwa mawasiliano ya simu ya Rais Trump

James Clapper
James ClapperPicha: Reuters/K. Lamarque

akisema hakukuweko agizo la mahakama ambalo lingaliruhusu jambo kama hilo kufanywa. "Ninafikiria ni kwa manufaa ya kila mmoja, manufaa ya rais wa sasa, manufaa kwa wademocrat, kwa warepublican na kwa manufaa ya taifa uchunguzi wa kina kufanywa dhidi ya madai haya kwa kuwa yanakanganyisha, na labda Warusi wanafurahia juhudi zao zinapozua mgawanyiko humu nchini."

Trump aliwasilisha madai yake kupitia ukurasa wake wa twitter siku ya Jumamosi bila ya uthibitisho zaidi akisema "Ni hali ya kudunisha kwamba Rais Obama alinasa mawasiliano yangu ya simu wakati wa uchaguzi”. Madai ambayo Obama aliyakanusha kupitia msemaji wake.

Ni wapi Trump alipata madai hayo?

Alipohojiwa na runinga ya ABC, naibu msemaji wa ikulu Sarah Huckabee Sanders alikataa kueleza ni wapi rais Trump alikotoa madai yake. Sanders alisema. "Tazama, ninafikiria yeye huenda nje ya habari ambayo ameiona, ambayo imemfanya kuamini kuwa haya yana uwezekano mkubwa. Na ikiwa kweli, basi itakuwa ni matumizi mabaya zaidi ya madaraka na shambulizi dhidi ya demokrasia, na Wamarekani wana haki kujua ikiwa hicho kilifanyika.”

Hata hivyo mwenyekiti wa Republican anayeiongoza kamati teule ya ujasusi bungeni Devin Nunes, amesema kamati yake itayashughulikia madai ya Trump, hasa baada ya ikulu ya Marekani kuliomba bunge kuyachunguza madai hayo.

Madai hayo yamezua cheche za ukosoaji huku wengi wakisema lengo la Trump ni kuyabadilisha mawazo ya watu dhidi ya misururu ya ufichuzi kuhusu mikutano au mahusiano ya washirika wake na maafisa wa Urusi.

Mwandishi: John Juma/AFPE/APE

Mhariri: Yusuf Saumu