1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani ruksa kujadiliana na Ugiriki

Admin.WagnerD17 Julai 2015

Bunge la Ujerumani Bundestag limeipa idhini serikali kuanzisha mazungumzo juu ya mpango wa uokozi wa Ugiriki, wakitii onyo lililotolewa na Kansela Angela Merkel kuwa hatua yoyote mbadala ingesababisha machafuko makubwa.

https://p.dw.com/p/1G0lE
Deutschland Bundestag Sondersitzung Griechenland
Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Wakati wajumbe 439 kati ya 598 wa Bundestag waliopiga kura kuhusu mazungumzo hayo wameunga mkono majadiliano kwa ajili ya mkopo wa uokozi wa euro bilioni 86 kwa Ugiriki, idadi kubwa ya wajumbe 191 wameyapinga.

Idadi hii ni kubwa ikilinganishwa na wabunge 32 ambao mwezi Februari walipinga kurefushwa kwa mpango wa mwisho wa uokozi wa Ugiriki. Wabunge wengine 40 wamejizuwia kupiga kura, lakini mgawanyo wa kura kwa msingi wa vyama ulikuwa bado haujatolewa.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa Wagiriki wakati wote wa mgogoro wa kiuchumi wa taifa lao.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa Wagiriki wakati wote wa mgogoro wa kiuchumi wa taifa lao.Picha: picture-alliance/dpa/W. Krumm

Katika hotuba yake kwa bunge mapema, Kansela Merkel aliwasihi wabunge kuunga mkono mazungumzo ya mkopo mpya kwa Ugiriki, na kuonya kuwa Ugiriki ingekumbwa na machafuko na vurugu ikiwa makubaliano ya msaada mpya hayangefikiwa.

"Tutakuwa na hatia ya uzembe mkubwa ikiwa hatutajaribu angalau njia hii, alisema Merkel akimaanisha mpango huo mpya, ambao ulifikiwa siku ya Jumatatu baada ya saa 17 za majadiliano kati ya viongozi wa kanda ya euro na Ugiriki.

"Nafahamu kuwa kuna mashaka na wasiwasi mkubwa, iwapo njia hii itafanikiwa. Iwapo Ugiriki itakuwa na nguvu ya kuendelea na njia hii kwa muda mrefu, alisema kansela huyo na kuongeza kuwa hakuna anayeweza kupuuza wasiwasi huu, "lakini jambo moja nililo na uhakika nalo ni kwamba ungekuwa uzembe wa hali ya juu iwapo tusingejaribu njia hii."

Upinzani unazidi taratibu

Muungano wa Merkel unaotawala - ambao unakijumlisha chama chake cha Christian Democratic Union CDU, washirika wao wa jimbo la Bavaria katika chama cha Christian Social Union CSU na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto SPD - wana wingi wa asilimia 80 katika bunge lenye jumla ya viti 631.

Pamoja na hayo, idadi kubwa ya wabunge wanaopiga kura ya hapana inaakisi upinzani unaozidi kuwa mkubwa miongoni mwa wapigakura wa Ujerumani dhidi ya kutumia fedha zaidi za walipakodi kuisaidia Ugiriki baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo ya vuta nikuvute kati ya nchi hiyo na wakopeshaji wake.

Wakati wa mjadala wa bunge la Ujerumani, Wagiriki waliandamana mjini Athens wakimlaani Schaeuble.
Wakati wa mjadala wa bunge la Ujerumani, Wagiriki waliandamana mjini Athens wakimlaani Schaeuble.Picha: DW/M. Fürstenau

Upo uwezekano mkubwa kwamba miongoni mwa waliopinga mazungumzo wemehusisha pia wanachama wa chama cha Merkel cha CDU na washirika wao wa CSU. Moja wa wapinzani wa msaada mpya wa Ugiriki kutoka chama cha CDU, Klaus-Peter Willsch, aliliambia bunge kuwa itakuwa vigumu kuanzisha mageuzi kwa sababu haiko bayana iwapo Ugiriki ina nia ya kutekeleza mageuzi hayo. Alisema tatizo liko kwa Ugiriki na linaweza tu kutatuliwa nchini Ugiriki.

Uchunguzi wa maoni uliyotolewa leo na televisheni ya umma ya Ujerumani umeonyesha kuwa asilimia 49 ya wapigakura wa Uejerumani wanapinga kufanyika kwa mazungumzo kuhusu mpango mpya wa uokozi, wakati asilimia 46 wanaunga mkono. Uchunguzi huo pia umebainisha kuwa asilimia 85 ya waliohojiwa wanataraji Ugiriki itategemea msaada kwa muda mrefu sana ujao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman