Bundesliga:Schalke-Hamburg sare 3:3
26 Oktoba 2009Katika Bundesliga-Bayer Leverkusen, imebakia kileleni mwa Bundesliga licha ya kumudu sare na Borussia Dortmund.
Mahasimu wao Hamburg pia walitoka suluhu na Schalke katika changamoto kati ya timu ya ngazi ya pili na ya tatu.
Chelsea, imeparamia tena kileleni mwa Premier League-ligi ya Uingereza baada ya kuichezesha Blackburn Rovers mabao 5-0.
Manchester United lakini, iliteleza mbele ya FC Liverpool ilipokandikwa mabao 2-0.
Stadi wa Mali, Seydou Keita, ametia mabao 3 kwa FC Barcelona katika ushindi wao wa mabao 6-1 dhidi ya Real zaragoza huko Spain.
Na Inter Milan, imebakia kileleni mwa Serie A-Ligi ya Itali.
Bundesliga: Bayer Leverkusen ingawa kwa wingi wa magoli tu ,imesalia kileleni mwa bundesliga mwishoni mwa wiki.Mahasimu wao Hamburg walio pointi sawa nao ingawa tofauti ya magoli,wakiongoza kwa mabao 2:0 kabla schalke kusawazisha :
Bao la dakika ya mwisho la Kevin Kuranyi liliokoa pointi 1 kwa Schalke jana na kuigandisha Hamburg iliopo nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi .Hamburg ikitazamiwa kuilaza Schalke na kuchupa hadi nafasi ya kwanza mbele ya Bayer Leverkusen.Mwishoe, lakini,Schalke, iliambia Hamburg: "Kutangulia kwa mabao 2 si kufika."
Kwani, Kevin Kuranyi, baada ya utamu wa bao lake la kwanza kumkolea, alirudi dakika ya mwisho ya mchezo na kutia bao maridadi la kichwa lililoinyima Hamburg pointi 3 nyumbani.Matokeo hayo yakabakisha Leverkusen ,kileleni mwa Bundesliga ,licha ya kuwa hata na wao hawakumdu zaidi ya suluhu ya bao 1- 1 na Burussia Dortmund ijumaa usiku.
Mabingwa mara kadhaa Bayern Munich walitkwa na jasho kabla kuzima dakika ya mwisho vishindo vya Eintracht Frankfurt.Ushindi wa Munich wa mabao 2-1, hatahivyo, haukuchangia sana kumaliza misukosuko ya kocha wao ,Mdachi, van Gaal.Alexander Meier, alilifumania kwanza lango la Bayern Munich na kuipa Frankfurt uongozi,lakini mdachi Arjen Robben,alisawazisha dakika 10 tu baadae.
Ikibainika kana kwamba, Frankfurt imemudu kuondoka na pointi 1 kutoka Munich, kocha Van Gaal, alitupa turufu yake mezani.Alimtoa mshambulizi mtaliana Luca Toni na kumwita Mbelgiji ,beki-mshahara Daniel van Buyten.Hii, iliwasangaza wengi Kwani, katika vitabu vya dimba, humbadilishi mshambulizi kwa mlinzi ukihitaji kushambulia zaidi na kushinda.
Mnamo dakika ya 88 ya mchezo-dakika 2 kabla firimbi ya mwisho kulia, mlinzi van Buyten alimuokoa kocha wake van Gaal kwa bao la kichwa lililookoa pointi 3 ilizohitaji Munich kujongelea kileleni.Van Gaal akasema baadae,
"Niligundua kuwa Luca Toni ,alikuwa hoi, amechoka.Nikijua kuwa, van Buyten, ni stadi wa kutia mabao kwa kichwa.....Nimebahatika sana leo kuona turufu yangu ya kubadilisha mchezaji imeshinda."
Munich haikuanza vyema msimu huu na kati ya wiki iliopita, walipatwa na msukosuko pia katika Chammpions league huko Ufaransa, walikozabwa mabao 2:1 na Girondins Bordeaux. Sasa Bayern Munich, inanyatia kuparamia tena kileleni kutoka ngazi ya 5 ya Ligi.
Ktika mapambano mengine, Stuttgart, imepatwa tena na mkosi ilipozabwa bao 1:0 na Hannover.Hoffenheim, ilitamba nyumbani kwa mabao 3-0 dhidi ya Freiburg.Changamoto kati ya mahasimu 2 wa mto Rhein,FC Cologne na Borussia Mönchengladbach ,ilimalizika suluhu 0:0 baada ya kikosi kikubwa cha polisi kushika zamu kuzuwia fujo kati ya mashabiki hasimu wa timu hizo2. pombe ilipigwa marufuku kuuzwa mjini Mönchengladbach ili kumpunga shetani wa dimba siku hiyo.
Tukigeukia Premier League-Ligi ya Uingereza,Frank Lampard, alipiga hodi mara 2 katila lango la Blackburn Rovers na kukaribishwa ndani na mwishoe, Chelsea ikaondoka na ushindi wa mabao 5:0.Na kwavile, FC Liverpool iliipiga kumbo Manchester united kwa mabao 2:0, Chelsea ilichupa hadi kileleni mwa Premier League.Fernando Torress-gombe-dume la Spain na David Ngog, walitia mabao ya Liverpool katika lango la Manu.
Arsenal ilifanya madhambi ilipoongoza kwa mabao 2, halafu ikazubaa na kuiachia West Ham kusawazisha .Hatahivyo, Arsenal iliparamia ngazi hadi nafasi ya 3 baada ya Tottenham Hotspur iliposakamwa kwa bao 1:0 nyumbani na Stoke City.sasa Tottenham imeteleza na kurudi nafasi ya 4.
Ama katika La Liga,Ligi ya Spain,Stadi wa Mali, Seydou Keita, alitia mabao 3 pekee katika mvua ya magoli 6 -1 Barcelona ilioinyeshea Real Zaragoza. Zlatan Ibrahimovic ,alitia mabao 2.
Real Madrid, ikiwa inaugua kwa kuumia kwa wachezaji wake wengi, ilitoka suluhu 0:0 na Sporting Gijon . Sevilla sasa iko nafasi ya 3 baada ya kuondoka sare 0-0 nyumbani na Espanyol.
Katika serie A-Ligi ya Itali, Inter Milan bado iko kileleni.Bao la bahati tu la Mghana Sulley Muntari na mkwaju wa "freekick" wa Wesley Sneijder,yalitosha kuzima vishindo vya Catania uwanjani San siro na kuagana kwa mabao 2:1.Mahasimu wao wa mtaani AC Milan, wameendelea kupata nafuu kwa ushindi pia wa mabao 2:1 dhidi ya Verona.
Mwandishi: Ramadhan Ali /DPAE
Mhariri: M.Abdul-Rahman
◄