1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga: Kombe klabu bingwa Afrika na riadha Monaco

Ramadhan Ali12 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CHYi

Tukianza na Bundesliga-Ligi ya ujerumani, mabingwa Bayern munich walitoka nyuma hapo jumamosi na kuwatimua mahasimu wao wakubwa mkoani Nüremberg kwa mabao 2:1.Na sasa Munich, hawakushindwa mara 13 mfululizo.Ilikua Nuremberg lakini, ilioufumania kwanza mlango wa Munich pale kipa oliver Kahn,alipofanya kosa mnamo dakika ya 20 ya mchezo na Javier Pinola akatia bao.Bayern Munich lakini, haikuchelewa kujibu kwani Paolo Guerriero alisawazisha haraka.Bayern Munich ikicheza bila ya mshambulizi wao Roy makaay ,iliondoka na ushindi kufuatia bao la pili la kichwa na Michael Ballack.

FC Cologne iliotangaza juzi itayari kumfungisha mkataba satdi wake chipukizi Lukas Podolski wa hadi miaka 10 akitaka, ilizabwa mabao 2:1 jana na Borussia Dortmund.Lars Ricken ndie aliepiga hodi mara 2 katika lango la Cologne na kuitikiwa karibu.Kwanza kupitia mkwaju wa penalty na halafu kwa bao la kichwa.Cologne, iliamka dakika za mwisho ilipotia bao mnamo dakika ya 92 ya mchezo-bao alilotia Matthias Scherz.

Dortmund kwa kweli, ilistahiki ushindi kwavile tangu manzo ikihujumu lango la Cologne wakati cologne ikijilinda ikitumai alao kuondoka suluhu na pointi 1.

Kwahivyo, Munich inaongoza orodha ya ikiwa na pointi 12 kutoka mechi 4 na Werder Bremen na Hamburg ziko nyuma kwa pointi 2 kila moja .Schalke lakini, imerudi nyuma iko nafasi ya 4 baada ya kutoka sare jumamosi bao 1:1 na Bayer Leverkusen. Stadi wa Schalke,mzaliwa wa Ghana, Gerlad Asamoah anatazamiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha hadi miezi 2 baada ya kuumia jumamosi katika mpambano huo na Leverkusen.Asamoah hataweza pia kuichezea Ujerumani katika dimba la kirafiki dhidi ya China na Uturuki mwezi ujao.

Kocha wa Bayern Munich felix Magath amethibitisha lakini kwamba mshambulizi wao Roy Makaay aliedumia atakuwa fit kurudi uwanjani jumatano hii kwa mpambano wa Champions League-Kombe la klabu bingwa barani Ulaya kati ya Munich na Rapid Vienna ya Austria.

Franz Beckenbauer,wanaemuita ‘Kaiser Franz’-mfalme Franz, alisherehekea jana miaka 60 ya siku ya kuzaliwa .Gazeti la Handelsblatt likaandika hivi: “Ikiwa kuna yeyote anaetukuzwa mno katika dimba la Ujerumani bila ya shaka ni Franz Beckenbauer.”

Beckenbauer akiwa nahodha wa Bayern Munich alishinda kombe la klabu bingwa barani Ulaya miaka ya 1970,akaiongoza Ujerumani kutwaa Kombe la dunia kama nahodha 1974 nchini Ujerumani na kama kocha 1990 mjini Roma.Ni yeye alieipiku Africa kusini na kuleta tena Kombe la dunia Ujerumani mwakani .Beckenbauer ndie mwenyekiti wa kamati ya maandalio ya kombe lijalo la dunia.

Katika Ligi ya Spain, mshambulizi wa Kamerun,Samuel Eto’o alipiga nae hodi mara 2 katika lango la Real Mallorca hapo jana na kuipa ushindi FC Barcelona-mabingwa wa Spain.

Katika kombe la klabu bingwa barani Afrika,mabingwa Enyimba wameshafungishwa virago na kupigwa kumbo nje ya Kombe hili baada ya kulazwa jana kwa mabao 2:1 na Al Ahly ya Misri.

Enyimba ya Nigeria ilioiigiza TP Mazembe kutwaa Kombe la africa mara 2 mfululizo, ilikuwa njiani kuvunja rekodi kulinyakua Kombe hilo mara tatu mfululizo.Lakini,Al Ahly mabingwa wa zamani wamewatia munda.Enyimba jana walihitaji sare ili kubakia nafasi ya pili nyuma ya viongozi wa kundi Al Ahly baada ya Raja Casablanca ya Morocco kuitimua Ajax cape Town kwa mabao 3-0 huko Afrika kusini.

Mbali na zawadi ya dala milioni 1 kwa mshindi wa Kombe hili,mabingwa wan aiwakilisha Africa katika Kombe la dunia la klabu bingwa huko Japan desemba mwaka huu.Afrika ikipambanishwa na klabu bingwa ya Asia katika hatua ya robo-finali.

Stadi wa Chelsea,Didier Drogba ametishia kutoichezea tena timu ya Taifa ya Ivory Coast kutokana na jinsi mashabiki waliokasirika walivyoifanyia timu ya Taifa iliposhindwa nyumbani na simba wa nyika-Kamerun, jumapili iliopita.

Drogba ametishia kwamba, hali kama hiyo ikizuka tena , hatakabili hatari kwenda Abidjan kuichezea timu ya taifa.

Wachezaji wa ivory Coast-tembo- walitukanwa na kutishiwa kupigwa na baadhi ya mashabiki walioghadhibika kwa kukosa kucheza katika Kombe lijalo la dunia.

Nayo gabon imemtimua kocha wa timu ya taifa mbrazil Jairzinho-alieichezea Brazil katika Kombe la dunia, 1970 mjini Mexico.hii inatokana na kupigwa kumbo kwa gabon katika kinyan’ganyiro cha kuania tiketi za kombe la dunia ilipolazwa na Angola mabao 3:0 jumapili iliopita.

Bingwa wa olimpik wanawake wa masafa ya mita 5000 kutoka Ethiopia, Meseret Defar ameshinda mbio za mita 3000 na 5000 mwishoni mwa wiki na kuondoka Monaco na kitita cha dala 60.000.Defar alimshinda muethiopia mwenzake bingwa wa dunia Tirunesh Dibaba baada ya kutimka mbio kwa kasi hapo ijumaa katika masafa ya mita 5000 wanawake.