Bundesliga: Chipukizi wa kuwatazama msimu wa mwaka 2019-20
Bundesliga imekuwa ligi inayopendwa na wachezaji wachanga wanaotaka kuimarika kimchezo. Huku ikiwa Jadon Sancho na Kai Havertz washajijengea majina, wachezaji wengi chini ya umri wa miaka 21 sasa wako tayari kuibuka.
Kai Havertz, 20, Bayer Leverkusen
Nyota wa kizazi kijacho cha Ujerumani. Havertz ashacheza mechi 88 katika Ligi Kuu ya Ujerumani na kufunga mabao 24. Ana ujuzi wa ajabu wa kiufundi, anacheza kwa miguu yote miwili na ana uwezo wa kuunda nafasi za kufunga na kufunga mwenyewe. Havertz amesema atasalia kuwa mchezaji wa Leverkusen msimu huu ingawa ni wazi kuwa hatocheza hapo kwa muda mrefu. Bayern Munich wamevutiwa kwa muda mrefu.
Jadon Sancho, 19, Borussia Dortmund
Wengi walitaka kujua itakuaje kijana Muingereza kucheza Ujerumani, sasa ni kielelezo chema huku chipukizi wa Uingereza wakitaka kufuata nyayo zake. Winga huyo wa zamani wa Manchester City ana uwezo mkubwa na anafanya maamuzi mazuri kuzidi umri wake, ana kasi na amemakinika. Baada ya kupewa nafasi msimu wa mwaka 2017-18, alikuwa mmoja wa nyota msimu jana akifunga magoli 12 na kusaidia mengine 17.
Dayot Upamecano, 20, RB Leipzig
Beki huyo wa kati wa Ufaransa(juu kushoto) ni mwengine anayetazamiwa kufika kileleni. Upamecano ni mahiri kwa mipira ya kichwa na anasoma mchezo vyema. Anaweza pia kupeleka mipira katika kiungo cha kati. Amekuwa mmoja wa mabeki bora katika Ligi ya Ujerumani. Julian Nagelsmann atakuwa kocha mzuri kwake.
Ibrahima Konate, 20, RB Leipzig
Beki mwengine wa kati wa RB Leipzig ambaye anaweza kucheza vyema kwa mipira ya kichwa na chini. Konate alikuwa na msimu mzuri uliopita na aliishikilia nafasi yake vyema baada ya Upamecano kupata jeraha mwishoni mwa msimu. Chipukizi huyo wa Ufaransa amemuelezea Upamecano kama kakake na watatarajia kuendeleza mchezo wao wa kuridhisha msimu huu.
Alphonso Davies, 18, Bayern Munich
Winga huyo wa Canada alizaliwa katika kambi ya wakimbizi na akajiunga na Bayern mwezi Januari. Alishiriki mechi kadhaa kama mchezaji wa akiba na kwa ujumla alicheza dakika 74 na akafunga goli lake la kwanza dhidi ya Mainz. Kuondoka kwa Arjen Robben na Frank Ribery huenda kukatoa nafasi zaidi kwa Davies msimu huu hasa baada ya jeraha la mchezaji aliyelengwa na Bayern Leroy Sane.
Marcus Thuram, 21, Gladbach
Mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia na Ufaransa Lilian, alijiunga na Mönchengladbach mwezi Julai baada ya kuridhisha katik vilabu vya Ufaransa Sochaux na Guingamp. Kinyume na babake ambaye alikuwa mmoja wa mabeki mahiri wakati wake, Marcus ni mshambuliaji na anapenda kucheza katika wingi ya kushoto. Ana uwezo mkubwa wa kutamba na mpira na anaweza kupewa jukumu la Thorgan Hazard aliyehamia Dortmund.
Weston McKennie, 20, Schalke
Nyota iliyong'ara katika msimu wa kiza wa Schalke. Mckennie alikuwa nahodha wa Marekani katika mashindano ya Gold Cup msimu wa majira ya joto licha ya umri wake mdogo. Alicheza katika nafasi tofauti msimu uliopita wakati kocha wake Domenico Terdesco alipojaribu kutafuta mbinu ya kushinda ambayo hakuipata. McKennie amemkaribisha Mmarekani mwenzake David Wagner ambaye ameteuliwa kuwa kocha.
Evan N'Dicka, 19, Eintracht Frankfurt
Mfaransa mwengine N'Dicka aling'ara hakuzungumziwa sana msimu uliopita kwa kuwa washambuliaji watatu wa Frankfurt ndio waliogonga vichwa vya habari. Lakini beki huyu wa kati alikuwa na mchezo mzuri katika nusu ya pili ya msimu ambapo alishinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi kucheza mara ya kwanza katika Bundesliga mwezi Februari.
Josh Sargent, 19, Werder Bremen
Mshambuliaji huyu wa Marekani aling'ara mara alipopewa nafasi msimu uliopita ambapo alifunga kwa kichwa dakika mbili baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika mechi yake ya kwanza. Alimaliza msimu na mabao mawili kwenye ligi baada ya kucheza kwa dakika 205 tu na licha ya kukosa kutajwa kwenye kikosi cha Marekani cha Gold Cup kocha wake wa Bremen Florian Kohfeldt ameridhika naye.
Jann-Fiete Arp, 19, Bayern Munich
Baada ya kujiunga na Bayern mwaka mmoja kabla kutoka Hamburg, mshambuliaji huyo wa Ujerumani atatarajia kupata nafasi msimu huu wakati mabingwa hao watakapokuwa wanajaribu kumpunguzia mzigo Robert Lewandowski. Mshambuliaji mwenye kipaji, Arp aligonbga vichwa vya habari kwa kufunga katika mechi zake mbili za kwanza lakini alikuwa na wakati mgumu katika ligi ya daraja la pili msimu uliopita.
Tyler Adams, 20, RB Leipzig
Mmarekani wa tatu na mchezaji wa tatu wa Leipzig katika kundi hili, Adams aliwasili Leipzig kutoka tawi lao la New York mwezi Januari na alionekana kuingiliana vyema kimchezo katika kiungo cha kati cha Leipzig katika Bundesliga. Adams anaweza kucheza katikati au hata nyuma kidogo kama kiungo mkabaji.
Ademola Lookman, 21, RB Leipzig
Mmoja wa Waingereza waliofuata nyayo za Sancho, Lookman alikuwa na msimu mzuri alipokuwa kwa mkopo Leipzig. Mshambuliaji huyo anacheza sehemu yoyote ya mashambulizi na ni mfungaji ambapo alifunga mabao matano. Alifunga magoli 5 katika dakika 574 alizopata. Klabu yake ya Everton ilimkubalia ajiunge na Leipzig kwa kandarasi ya kudumu baada ya kupata nafasi finyu za kucheza hapo Goodison Park.
Achraf Hakimi, 20, Borussia Dortmund (loan)
Anakaribia kuingia msimu wa pili kwa mkopo kutoka Real Madrid, beki huyo alikuwa na maisha mazuri kama mchezaji na BVB ambapo alifunga na kusaidia kuunda mabao matatu katika mechi zake tano za kwanza. Akiwa anaweza kucheza pande zote mbili na akiwa ana uwezo sana wa kushambulia kuliko ulinzi, msimu wa Hakimi ulifikia mwisho kutokana na Jeraha la mguu.
Rabbi Matondo 18, Schalke
Winga huyo wa Wales amefuata nyayo za Sancho kutoka Man City na amejiunga na Schalke kwenye Bundesliga. Akiwa alisemekana kwamba ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi Man City, Matondo alifanikiwa kuingia mara kadhaa kama mchezaji wa akiba hapo Schalke mwaka jana. winga huyo atatarajia kupata nafasi nyingi zaidi za kucheza msimu huu.