1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSLES: Tofauti za kidiplomasia zazidi juu ya vita vya Lebanon

27 Julai 2006
https://p.dw.com/p/CG3X

Mgawanyiko wa kidiplomasia unazidi kuhusu njia za kuyamaliza mapigano nchini Lebanon, huku Ufaransa ikiutaka Umoja wa Mataifa upitishe azimio la haraka la kutaka mapigano yakome na Marekani kwa upande wake ikitoa vitisho vipya kwa Iran na Syria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Philippe Douste Blazy, ameitisha mkutano wa mawaziri wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mapema wiki ijayo kujadili azimio la kusitisha mapigano.

Mataifa ya Ulaya na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anataka juhudi zifanywe kuzijumuisha Syria na Iran katika kutafuta suluhisho la kisiasa nchini Lebanon.

Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amezionya Syria na Iran kwamba zitatengwa zaidi na jumuiya ya kimataifa zikijaribu kuziharibu juhudi za Marekani kuyamaliza mapigano kwa maslahi ya Israel.

Hii leo Condoleezza Rice amesema yuko tayari kwenda tena Mashariki ya Kati kujaribu kutafuta suluhisho lakini hakutaja ni lini.