1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Umoja wa Ulaya na NATO zaikosoa Korea Kaskazini

9 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD4R

Umoja wa Ulaya na shirika la kujihami la kambi ya magharibi, NATO, leo umeikosoa Korea ya Kaskazini kwa kufanya jaribio lake la kwanza la nyuklia, ukisema jaribio hilo linahatarisha usalama wa dunia.

Katibu mkuu wa shirika la NATO, Jaap de Hoop Schaeffer, amelilaani vikali jaribio hilo. Schaeffer amesema kitendo cha Korea ya Kaskazini ni dharau kwa jamii ya kimataifa.

Kwa upande wake kiongozi wa Umoja wa Ulaya anayehusika na sera za kigeni, Javier Solana, amesema jaribio hilo linahatarisha usalama na amani ulimwenguni kote.

´Tunahisi kitendo cha Korea ya Kaskazini kimeenda kinyume na kanuni zote tunazozilinda. Ningependa kusema pia kwamba jaribio la nyuklia ni habari mbaya kwa wananchi wa Korea ya Kaskazini. Serikali inatumia fedha nyingi kwa kitu ambacho hakitakuwa na faida yoyote kwa raia. Wananchi wa Korea ya Kaskazini wanaendelea kuteseka kwa njaa.´

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema Korea ya Kaskazini imejiingiza katika tatizo la kutengwa na jumuiya ya kimataifa.