BRUSSELS: Uchaguzi wa Zimbabwe wanukia.
30 Machi 2005Umoja wa Ulaya umeutaja uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika hapo kesho nchini Zimbabwe kuwa ni kiini macho.
Rais Robert Mugabe hataki wachunguzi wa kimataifa wasimamie uchaguzi huo amelalamika naibu wa mambo ya nchi za nje wa Luxembourg bwana nicolas Schmitt mbele ya bunge la Ulaya.
Marekani nayo pia inautia ila uchaguzi huo wa bunge nchini Zimbabwe.
Wakati huo huo rais Mugabe anawalaumu viongozi wa upinzani nchini humo kuwa wao ni vibaraka wa Uingereza.
Inatarajiwa kwamba chama tawala cha ZANU PF kinacho ongozwa na rais Robert Mugabe kitaibuka na ushindi katika uchaguzi huo.
Kwengineko mteule wa Marekani katika kiti cha rais wa benki kuu ya dunia Paul Wolfowitz amewasili mjini Brussels hii leo kwa mazungumzo na magavana wa benki kuu kutoka nchi za Ulaya.
Bwana Paul Wolfowitz na waziri mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Juncker hivi sasa wanazungumza na waandishi wa habari.
Umoja wa Ulaya unataraji mazungumzo ya leo yatafungua njia ya kuwakilishwa kwa nguvu zaidi nchi za umoja huo katika taasisi hiyo muhimu ya fedha.
Umoja wa Ulaya unapigania kushikilia angalao wadhifa wa makamo wa rais wa benki kuu ya dunia.
Nchi 25 za Umoja wa Ulaya zinawakilishwa na mawaziri wao wa fedha katika baraza la magavana wa benki kuu ya dunia.
Kuteuliwa kwa Paul Wolfowitz na rais George Bush ashikilie wadhifa wa rais wa benki kuu kumezusha manung’uniko miongoni mwa wanasiasa kadhaa wa Ulaya.