BRUSSELS: Sheria zaregezwa kuhusu nakisi ya bajeti
21 Machi 2005Mawaziri wa fedha wa nchi za Umoja wa Ulaya, katika mkutano wao mjini Brussels wamekubaliana na mpango utakaoregeza kwa muda sheria zinazodhibiti bajeti na ambazo huimarisha sarafu ya Euro.Mapatano hayo yanayotoa uhuru zaidi kwa serikali,nakisi zinapokuwa kubwa yamepatikana baada ya dai la Ujerumani kukubaliwa kwamba gharama kubwa zilizotokana na muungano wa Ujerumani lazima zizingatiwe.Duru kutoka Luxembourg ambayo sasa ni rais wa Umoja huo,zimesema mawaziri wa fedha walikubaliana kimsingi kuiandika upya "Katiba ya Utulivu na Ukuaji" ikitazamiwa kuwa itaidhinishwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao unaoanza siku ya Jumanne.Kwa miaka mitatu kwa mfululizo,nakisi za bajeti za Ujerumani na Ufaransa zilivuka kiwango kilichowekwa cha asili mia tatu.