1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wakutana Brussels

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
6 Aprili 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya kijeshi ya NATO wapo mjini Brussels kwa ajili ya mkutano ambapo wanajadili hatua zaidi za kuchukuliwa na muungano huo kuhusu mgogoro wa nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/49WwN
Annalena Baerbock (Buendnis 90/Die Gruenen), Bundesaussenministerin
Picha: Thomas Trutschel/photothek/imago images

Mawaziri hao wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa muungano wa kujihami wa NATO kwenye mkutano wao wanajadili pia juu ya maswala ya fedha, misaada ya kibinadamu na ya kijeshi kwa ajili ya Ukraine, na jinsi ya kutolewa misaada hiyo haraka kabla ya Urusi kuanza mashambulizi dhidi ya Ukraine yanayotarajiwa katika eneo la Donbas. Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema Urusi haijakata tamaa katika mashambulizi yake nchini Ukraine na kwamba inajipanga kufanya operesheni ya kijeshi kwa mara nyingine tena kwa ajili ya kulichukua kabisa eneo la Donbas katika wiki zijazo.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Yves Herman/AFP/Getty Images

Stoltenberg amesema katika wiki zijazo, Urusi inajipanga kuingia katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine kujaribu kulidhibiti eneo lote la Donbas na kisha kuweka daraja litakalo unganisha eneo hilo na Crimea ambayo inalikaliwa kimabavu na Urusi. Kwa hii ni awamu muhimu katika hivi vita. Stoltenberg ameeleza kwamba washirika wa NATO wamedhamiria kutoa msaada zaidi kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na silaha za kupambana na vifaru, mifumo ya ulinzi wa anga na vifaa vingine.

Katika kijiji cha Krasnopillia kilicho karibu na eneo la mpaka wa Urusi na Ukraine vikosi vya Ukraine tayari vimeanza kujiandaa kukabiliana na majeshi ya Urusi iwapo yataingia huko. Afisa mkuu wa jeshi la Ukraine aliye katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajua kwamba vikosi vya Urusi vinajiimarisha ili kulishambulia eneo hilo lakini wako tayari kwa mapambano hayo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NATO kwenye mkutano mjini Brussels
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NATO kwenye mkutano mjini BrusselsPicha: Olivier Douliery/AFP

Raia wametakiwa kuhama na kwenda katika eneo la magharibi na hapo jana mlolongo mrefu wa magari upatao kilomita tatu ulionekana kwenye eneo kilipo kituo cha ukaguzi, huku maelfu ya wakaazi wengine wakipanda treni na kuondoka kutoka kwenye kijiji cha Krasnopillia. Mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili hadi sasa hayajaenda popote, ingawa Moscow inasema iko tayari kuendelea nayo.

Vyanzo: RTRE/AFP