Brexit na vizibao vya manjano magazetini
26 Novemba 2018Tunaanzia na makubaliano ya Brexit ambayo licha ya kuungwa mkono na viongozi wa mataifa 27 yaliyosalia ya umoja wa Ulaya, hakuna uhakika kama yataidhinishwa na wabunge wa Uingereza. Gazeti la Badische Zeitung linaandika: "Kuna uwezekano mkubwa kwamba makubaliano hayo, yanayotajwa kuwa" bora zaidi" yasiungwe mkono na walio wengi bungeni. Kwa hivyo hakuna sababu ya kushangiria. Wapinzani wakubwa wa Brexit wanaamini bora kutokuwa na makubaliano kuliko haya yaliyofikiwa. Lakini wanaotea enzi za kale za himaya ya Uingereza-wamesahau tuko katika ulimwengu wa mtandao, karne ya 21. Anaepalilia vurugu anacheza na maisha ya binaadam.
Gazeti la Freie Presse linahisi makubaliano ya Brexit hayastahili kushangiriwa. Gazeti linaendelea kuandika: "Siku ya jana imefungua enzi mpya kwa Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya unabidi ukabiliane kwa moyo wa kijasiri na maadui wanaozidi kuongezeka. Mpaka iliyo wazi, miongo kadhaa ya amani, neema na utawala unaoheshimu sheria vinatishiwa na sio tangu kadhia ya Brexit ilipoanza."
Vizibao vya manjano vyafanya fujo Ufaransa
Waandamanaji wa Ufaransa wanaolalamika dhidi ya kupandishwa kodi ya mafuta -maarufu kwa jina "vizibao vya manjano" wamepambana na vikosi vya usalama katika eneo mashuhuri la mjini Paris-Champs Elysée. Gazeti la "Badische Neuste Nachrichten linaandika kuhusu malalamiko ya wafaransa dhidi ya mageuzi ya kiuchumi: "Vizibao vya manjano wanataka kutoa joto lao la moyoni dhidi ya rais Emmanuel Macron wakilalamika dhidi ya kile wanachokiita "kiburi chake"-lakini njia kali wanazotumia hazikubaliki. Sayari ya Mshtarii au Jupiter kama Macron alivyowahi wakati mmoja kujiita anabidi haraka arejee duniani kama anataka kuuokoa mhula wake."
Kinyang'anyiro cha kuania nafasi ya mwenyekiti wa chama cha CDU
Mada yetu ya mwisho inahusiana na mapambano ya kuania wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha Christian Democratic Union-CDU, uchaguzi mkuu wa chama hicho utakapoitishwa mapema mwezi unaokuja. Gazeti la "Der neue Tag linaandika: "Wafuasi wa CDU wataamua decemba saba kuhusu mwongozo mpya kwa chama chao ambacho kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wananchi kinazidi kupoteza sifa zake. Na mwongozo mpya hautowezekana pindi Friedrich Merz akichaguliwa. Sio fedha nyingi anazolipwa ndizo zitakazomfanya astahiki kumrithi kansela Merkel na sio matamshi yake makali pia. Hali ya kutoaminika ndio itakayomponza.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman