1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil yazindua mipango ya kupambana na Zika

25 Machi 2016

Brazil inaendelea na maandalizi ya tamasha maarufu kabisa la michezo duniani. Waziri wa afya amezindua mipango ya kuwahudumia wanamichezo na mashabiki watakaohudhuria Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro mwezi Agosti

https://p.dw.com/p/1IJz1
Brasilien - Maßnahmen gegen Zika Virus - Rio de Janeiro
Picha: Reuters/P. Olivares

Hofu kubwa ya kiafaya kabla ya Michezo hiyo inaendelea kuwa ni maambukizi ya virusi vya Zika na maradhi mengine kama vile homa ya Dengue na Chikungunya ambayo yanasambazwa na aina Fulani ya mbu. Waziri Marcelo Castro amefafanua kuwa idadi ya mbu hao katika miezi ya kipupwe ni ndogo "tunafanya juhudi kubwa hapa Brazil kupambana na mbu huyu. Tunalenga hasa mjini Rio de Janeiro. Tutaimarisha juhudi zetu hata zaidi mjini Rio de Janeiro, ili kujiandaa katika njia nzuri kwa Olimpiki. Tutalenga katika maeneo yote watakakoishi wanamichezo wa Olimpiki, ambako mashindano yatafanyika, ambako watu wataishi. Bila shaka tutafanya kazi jumla, lakini kwa kuyaangazia maeneo haya".

Serikali ya Brazil imezindua operesheni kali ya kuwaangamiza mbu hao kwa kuwaajiri maelfu ya wanajeshi kupuliza kemikali za kuwaua na kuuhamasisha umma namna ya kuangamiza mazingira ya wadudu hao katika maeneo ya makazi. Castro amesema maabara 30 mpya zitazinduliwa kwa ajili ya michezo hiyo ili kuwafanyia vipimo watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya Zika na maradhi mengine "tutaweka vifaa vya kisasa katika maabara zetu ili tuweze kufanikisha vipimo haraka iwezekanavyo. Ili tuweze kusema, kwa mfano, kama mtu ana homa, nini chanzo chake? Dengue, Chikungunya, Zika, homa ya uti wa mgongo, au mafua. Maabara zetu yamewekwa vifaa bora kwa tamasha hili".

Wakati huo huo, kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro imesema ina matumaini kuwa hakuna maeneo na viwanja vya mashindano hayo vinavyohusishwa na kashfa ya ufisadi inazozikumba sekta za siasa na biashara nchini humo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu