Brazil yaizima Italia katika kundi A
23 Juni 2013Brazil ilishinda kundi A la mechi za Conferederations katika mchuano wa kusisimua ambao walishinda mabao manne kwa mawili dhidi ya Italia wakati timu hizo mbili kuu za kombe la dunia zilipokabana koo.
Timu zote mbili zilifahamu kuwa zitakuwa katika nusu fainali, lakini zawadi kubwa ya mechi ya jana ya kukwepa kucheza katika mchuano kati washindi wa kundi B Uhispania iliwaendea Selecao. Mabao ya Brazil yalifungwa na Dante, Neymar na Fred ambaye alitikisa wavu mara mbili, huku nao Emanuele Giaccherini na Giorgio Chiellini wakiifungia Italia. Neymar na Abate walibadilishana masumbwi katika kipindi cha kwanza hadi Muitaliana huyo akaondoka uwanjani akiwa na jeraha.
Mexico ambao tayari wametimuliwa katika dimba hilo walikwepa kumaliza katika nafasi ya mwisho katika kundi lake, kwa kuwachapa Japan mabao mawili kwa moja katika mechi nyingine.
Mabao yote mawili yalifungwa kwa kichwa na mshambuliaji Javier Chicharito Hernandez ambaye pia alishindwa kufunga penalti katika kipindi cha pili cha mechi hiyo. Goli la Japan lilifungwa na Shinji Okazaki. Scolari amesema sasa wako tayari kwa mechi ya nusu fainali ambapo watakutana na nambari mbili wa kundi B. amesema kikosi chake kiko tayari na kuwa kitasaidiwa pia na mashabiki wa nyumbani.
Naye kocha wa Italia Cesare Prandelli amesema wakati matokeo yalipokuwa matatu kwa miwili, walistahili kutoka sare, lakini ikawa vigumu kwa sababu ya wachezaji wenye uwezo mkubwa wa Brazil. Hata hivyo alisema ameridhika na matokeo ya vijana wake kwa sababu walionyesha mchezo mzuri katika kipindi cha pili. Amesema wako tayari kwa nusu fainali dhidi ya Uhispania.
Hii leo usiku, Uhispania itashuka uwanjani kupambana na mabingwa wa Afrika Nigeria wakati Uruguay ikiwakaribisha Tahiti katika mechi za mwisho za awamu ya makundi katika dimba la Confederations. Victor Valdes atakuwa mlinda lango wa Uhispania katika mchuano wa leo, ijapokuwa kocha Vicente del Bosque amesema kikosi chake kitakuwa kile kilichocheza mechi ya ufunguzi.
Uhispania ni kama wamejikatia tayari tikiti ya kucheza nusu fainali na watacheza na Italia Alhamisi wiki ijayo. Hata kam watashindwa na mabingwa wa Afrika, Nigeria watalazimika kushinda kwa zaidi ya mabao manne kwa sababu Uruguay ni kama watawashinda Tahiti katika mechi nyingine ya leo. Nahodha wa Super Eagles Victor Enyeama amesema kuwa vijana wake wataingia uwanjani bila uwoga wowote wakati watakapokabana koo an mabingwa wa Dunia Uhispania.
Mwandishi. Bruce Amani/DW/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo