Brazil yaivumbua Afrika, kibiashara
25 Septemba 2009Lengo la Rais wa Brazil, Luiz Inacio "Lula" da Silva ni kuwa na jeografia mpya katika biashara ya kimataifa. Rais huyo, ambaye zamani alikuwa kiongozi wa chama cha wafanya kazi, anataka Brazil ifungamanishwe kwa ubora zaidi na nchi nyingine zinazoendelea na zile zinazoinukia; kama vile alivosema mwaka 2004 katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Biashara ya Dunia huko Sao Paulo. Hata hivyo, yeye anataka nchi yake iendelee kusafirisha bidhaa zake kwa nchi za viwanda, lakini uwezekano mpya lazima ufunguliwe. Rais Lula da Silva anasema wao wanataka kuendeleza ushirika ambao utaweza kuingiza uchumi wa nchi za Kusini mwa sayari yetu hii ya dunia.
Brazil inauza bidhaa zaidi kwa nchi zinazoendelea na zile zinazoinukia kuliko kwa nchi za kaskazini ya dunia. Nchi ya tatu inayofanya biashara kwa wingi na Brazil ni China, ikiwa nyuma ya Marekani na karibu katika kiwango hicho hicho na nchi jirani ya Argentina. Licha ya China, ni hasa Afrika inaowavutia wafanya biashara wa Brazil, bara ambalo limetoa watumwa wa zamani ambao waliopata makao huko Brazil.
Mwenyewe Rais Lula wa Brazil amefanya ziara kumi na moja katika Bara la Afrika na ameashiria kwamba nchi yake inakaliwa na watu wengi kabisa wenye asili ya Afrika nje ya Bara lenyewe la Afrika. Pia wakala wa serekali wa kuendeleza usafirishaji wa bidhaa kwenda ngambo, APEX, umezidisha shughuli zake. Mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba, ujumbe wa wafanya biashara wa Brazil ulitembelea Afrika Kusini. Mauricio Manfre, mkuu wa miradi ya APEX alisema fikra yao ni kuujenga na kuupanua uhusiano huo.
Katika miaka kumi iliopita bidhaa za Brazil kwendea nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimezidi karibu mara nane. Mwaka jana gharama za bidhaa hizo zilifikia zaidi ya dola bilioni kumi au asilimia tano ya bidhaa za Brazil zilizosafirishwa ngambo. Angola ikinunua bidhaa za gharama ya dola bilioni mbili ilikuwa nambari moja, ikifuatiwa na Afrika Kusini ilioagizia bidhaa za gharama ya dola bilioni 1.8 na Nigeria dola bilioni 1.5.
Katika wakati huu wa mizozo ya kifedha na kiuchumi duniani, masoko mepya ya Afrika ni jambo linalokaribishwa. Nchi zinazoinukia hazijaathirika sana na mzozo wa sasa wa kiuchumi duniani, nchi hizo zimebakia kuwa masoko ya kuvutia kwa makampuni madogo madogo, kama yale ya Brazil ambayo yanatoa bidhaa kwa tabaka za watu wa kati na kati na wale wa chini. Barani Afrika na katika Mashariki ya Kati tabaka za watu hao ndio wateja wa bidha hizo.
Wakati China inanua thuluthi mbili ya mali ghafi kutoka Brazil, kama vile Soya na chuma, na kuacha bidha ambazo tayari zimeshatengenezwa, bidhaa za Brazil zinaopelekwa Afrika ni za aina nyingi. Ni thuluthi moja tu ndio mali ghafi, thuluthi mbili iliobaki ni bidhaa zilizokwishatengenzwa: kutoka vitambaa, fanicha hadi mashine za kilimo. Nchi za Kiafrika bado hazijaweza kuendeleza viwanda vyao, na ndio maana Waafrika wengi wananua bidhaa za kiviwanda kutoka Brazil, hayo yalisemwa na Carlos Abijaodi, bingwa wa masuala ya biashara huko Brazil. Brazil ni karibu na Afrika, watu wa nchi hizo wana tabia za namna moja, na katika nchi kama vile Angola na Msumbiji watu wanazungumza Kireno kama wale wa Brazil.
Mshirika mkubwa wa kibiashara wa Brazil katika Afrika ni Angola. Katika nchi hiyo inayotoa mafuta na ambayo katika miaka iliopita uchumi wake umeweza kupanda kwa zaidi ya asilimia kumi, makampuni mengi ya Brazil yanawekeza. Kampuni ya mafuta ya Petrobras, ikimilikiwa nusu na serekali, inatafuta mafuta katika mwambao wa Angola, na kampuni ya ujenzi ya Odebrecht inajenga mabarabara. Pia kampuni ya Camargo inajenga kiwanda kipya cha saruji chenye gharama ya dola milioni 370.
Katika miaka ijayo, pia Msumbiji, nchi yenye wakaazi wengi katika maeneo ya Afrika yanayozungumza lugha ya Kireno, itapewa umbele zaidi na Brazil. Katika nchi hiyo, kampuni ya zamani ya Brazil ya uchimbaji wa migodi, Vale, imewekeza dola bilioni 1.3 kuchimbua makaa huko Moatize, katikati ya Msumbiji. Moatize ni mgodi mkubwa kabisa wa makaa duniani, na inasemakana unaweza ukatoa makaa kwa zaidi miaka 100 ijayo.