Brazil yaifunga Tanzania mabao 5-1
7 Juni 2010Katika mchezo huo uliyochezwa jijini Dra es Salaam na kuonesha katika nchi takriban zote duniani, Brazil ilipata mabao yake kupitia kwa Robinho na Ramires waliyopachika mabao mawili kila mmoja, huku Kaka akifunga moja.Bao hilo la Kaka ni la kwanza kufunga akiwa na timu hiyo katika kipindi cha takriban mwaka mmoja.
Hiyo ni mechi ya kwanza kubwa kwa Tanzania, ambayo imecheza siku moja tu babada ya kutolewa na Rwanda katika michuano ya kuwania nafasi ya kucheza katika fainali za Afrika kwa wachezaji wasiyo wa kulipwa.
Bao pekee la Tanzania lilifungwa na Jabir Aziz dakika tatu kabla ya mpira kumalizika na ni bao ambalo limefuta rekodi ya Brazil kucheza mechi sita mfululizo bila ya wavu wake kuguswa.Timu ya mwisho kutikisa wavu wa Brazil ilikuwa Bolivia Oktoba mwaka jana.
Wachezaji wa Tanzania walijitahidi kuonesha kandanda la kuvutia, dhidi ya timu bora kabisa duniani, lakini walionekana kutokuwa na nguvu za kutosha kuweza kuwakabili wachezaji wa timu hiyo.Tanzania inakamata nafasi ya 109 katika orodha ya ubora duniani.
Katika mechi hiyo, Brazil haikumcheza mlinda mlango wake nambari moja Julio Cesar, ambaye katika mechi na Zimbabwe alipata maumivu ya mgongo.
Mwandishi: Aboubakary Liongo