Brazil watafuta kulipiza kisasi
26 Machi 2018Kipigo hicho cha magoli saba walichopewa Brazil kilikuwa katika udongo wao wa nyumbani kwenye kombe la dunia lililopita?
Jumanne ni siku ya mwisho ya mechi za kirafiki za kimataifa kabla timu zitakazoshiriki kombe la dunia kutangaza vikosi vyao vya awali mnamo mwezi Mei huku vikosi vya mwisho vya wachezaji 23 vikitarajiwa kuwasilishwa Juni 3. Mojawapo ya mechi ambayo itakuwa inaangaliwa kwa karibu na mashabiki wa soka ni ile itakayowapatanisha Ujerumani na Brazil mjini Berlin.
Timu zote mbili zitakuwa zinatarajia matokeo mazuri ila the Selecao wa Brazil watakuwa watakuwa wanautaka ushindi zaidi baada ya kile kipigo cha magoli 7-1 walichopewa na Ujerumani huko Belo Horizonte miaka minne iliyopita katika kombe la dunia.
Brazil na Ujerumani wote wanapigiwa upatu kuebuka mabingwa wa dunia huko Urusi na Brazil wameonekana kuzinduka kutoka kwenye aibu waliyoipata mikononi mwa Ujerumani tangu kocha wao Tite achukue uongozi kwani ushindi wao wa tatu bila dhidi ya Urusi Alhamis iliyopita ni jambo linaloonesha kwamba ni timu ambayo haistahili kudharauliwa.
Tite amesema ni muhimu sana kwa vijana wake kuchuana na Ujerumani ila kipigo walichopewa miaka minne iliyopita ni jambo la zamani na sasa wako tayari kuangalia yaliyo mbele yao.
Brazil watamkosa mchezaji nyota wao Neymar ambaye anauguza jeraha la mguu nao Ujerumani watawapumzisha Mesut Özil na Thomas Müller.
Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/AFPE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman