BRAZIL NDIO MABINGWA WAPYA WA CONFEDERATIONS CUP
30 Juni 2005Kati ya wiki hii, mashabiki wa dimba kote ulimwenguni walijionea finali ya kukumbukwa mno ya Kombe la mashirikisho-Confederations Cup ilioitawaza Brazil mabingwa mjini Frankfurt,Ujerumani.
Brazil iliichezesha Argentina kindumbwe-ndumbwe na mwishoe kuizaba mabao 4:1.Huo ukawa ushindi mkuu wa Brazil mbele ya Argentina tangu kupita miaka 37.Sasa Brazil sio tu mabingwa wa dunia, Copa Amerima bali pia wa Kombe la mashirikisho wakati mmoja.
Kombe la mashirikisho kabla kuja Ujerumani, lilikuwa bado halikukubalika miongoni mwa mashabiki.Wiki 2 zilizopita lakini,limebainisha limekomaa na lina msisimko wake ajabu kama kombe hasa linalotufungulia pazia la Kombe la dunia.
Hata rais wa FIFA Sepp Blatter kwamba Kom be hili ambalo awali lilikua kama mtoto anaetambaa sasa limesimama kwa miguu yake 2.Mchezo wa timu zote 8 zilizoshiriki kuanzia mabingwa wa Afrika Tunesia,mabingwa wa ulaya, ugiriki, wa asia Japan, Australia,Argentina ,Brazil na wenyeji Ujerumani,kila mmoja alipania kushinda Kombe hili.
Confederations Cup limejionea jumla ya mabao 56 mnamo muda wa wiki 2 katika mechi 16.Hii ni sawa ya mabao 3.5 kila mchezo.Miongoni mwa mabao maridadi ajabu ni yale 2 aliyotia msham,bulizi wa Brazil Adriano –kwanza dhidi ya Ugiriki na jana dhidi ya Argentina kwa kufyatua mkwaju mkali kuitoka kiasi cha masafa ya mita 30.
Brazil imeshinda kwa staili yake ya kuhujumu iliowapatia jumla ya mabao 12 katika mechi zao 5.Hii imemfanya kocha wao Carlos Alberto parreira kuungama kwamba Brazil sasa ndio ya kutarajiwa kuibuka mwakani mabingwa wa dunia kwa mara ya 6.
Akiwa na Adriano,Ronaldinho,kaka,Robinho na Ronaldo ambae hakushiriki katika Kombe hili,Brazil ina mkuki mkali kabisa kwa kila adui –na Argentina wiki hii iliumizwa vibaya na mkuki huo.
Tayari Ronaldo ameungama kwamba nafasi yake katika kikosi cha timu ya Brazil sasa haina uhakika,lakini anabakia na uamuzi wake kwamba kwake ilikua bora apumzike na asishiriki katika Kombe hili.
Adriano ametia jumla ya mabao 5 na ameibuka mtiaji mabao mengi kabisa katika Kombe hili.Amevalishwa kiatu cha dhahabu na kuchaguliwa mchezaji bora wa Confederations Cup.
Kwahivyo, Ronaldinho,Adriano,kaka na robinho wamebainisha kwamba Brazil ni ya kuitumainia mwakani kutwa KOMBE LA DUNIA;LAKINI KUNA WENGINE AMBAO HAWANA UMAARUFU KAMA HUO LAKINI WAMEJITOKEZA KATIKA Kombe hili-miongoni mwao ni Cicinho,mbeki mshahara aliejaza pengo la Cafu na pasi zake maridadi ziliongoza kuizima Argentina.
Robinho, chipukizi wa miaka 21 ameelezea juzi hamu yake ya kuiacha Santos klabu yake na ya zamani ya Pele ili ajiunge na Real Madrid ya Spain.Klabu yake ya Santos imeweka kima cha Euro milioni 50 kwa klabu yoyote inayopiga hodi kumnunua chipukizi wao Robinho waliomtawaza “Pele mpya”.
Robinho anatakiwa na klabu mbali mbali za ulaya pamoja nao Arsenal London.Mkataba wa Riobinho na Santos lakini unadumu hadi 2008.Mwezi uliopita, Roberto Carlos alifichua kwamba mpango wa kumhamishia Robinho Real takriban umekamilika.
Argentina nayo yastahili sifa ,kwani ilichangia mno kulisisimua Kombe hili la Confederations Cup.uiliitoa Tunesia kwa mabao 2:1,ilitoka suluhu na Ujerumani 2:2 mjini Nuremberg na wakabainisha wangewanyoa tena bila maji mabingwa wa dunia Brazil kama walivyofanya mjini Buenos Ares wiki 3 nyuma.Na ingawa kati ya wiki hii walishikishwa adabu na Brazil,walionesha wamechoka baada ya msimu mrefu uliofikia kilele chake kukata tikiti yao na mapema ya Kombe la dunia na finali ya Confederations Cup.
Kwa kanda ya Amerika Kusini na kati, timu 3 zilitia fora usoni katika Kombe hili:Brazil,Argentina na Mexico iliotolewa na Ujerumani kwa mabao 4-3 baada ya kurefushwa mchezo.
Na wakati baadhi ya mastadi wao wakubwa hawakuja ujerumani kwa Kombe hili kama vile Ronaldo,Roberto Carlos na Cafu upande wa Brazil;Hernan Crespo ,Roberto Ayala na Kily Gonzales upande wa Argentina ,wengine wamejaza pengo lao tena barabara kuliko ilivyotazamiwa.timu ya Mexico ,kipa wao Oswalado Sanchez na mchezaji wa kiungo Zinha watakumbukwa mno.
Kwa upande wa wenyeji Ujerumani,hata wakosoaji wa kocha Jürgen Klinsmann wanaungama sasa kwamba tangu ashike usukani kutoka kwa Rudi Völler,ameifikisha mbali timu ya Ujerumani.Amewajenga wachezaji wapya na wachanga kama Lukas Podolski,Bastian Schweinsteiger na Mertesacker wako tayari kwa Kombe la dunia.Lakini Ujerumani mpya baada ya Kombe la Ulaya ikiwa na makipa 2 maarufu wanaoshinda Oliver Kahn na Jens Lehmann wa Arsenal,ina mashaka nyuma:Timu ikiruhusu mabao 11 katika mechi 5 za Kombe hili lazima ingiwe na wasi wasi na hasa ikikumbana na mizinga ya timu kama Brazil ya akina adriano,Robinho,Kaka na Ronaldo.
Klinsmann ana mwaka mmoja kutia kiraka katika ngome yake.
Japan mabingwa wa Asia ambao kama Argentina wameshakata tiketi yao ya kombe la dunia,iliacha ukumbusho mwema katika Kombe hili na watakaporudi wajapani mwakani,hakuna atakaewatoa maanani.Waliwashinda mabingwa wa Ulaya Ugiriki,ikalazwa chupuchupu 2:1 na Mexico kabla kutoka suluhu 2:2 na mabingwa wa dunia Brazil.
Australia mwanzoni ilinawiri ilipoizima Ujerumani n a mwishoe kulazwa kwa mabao 4-3.Australia ikalazwa kwa mabao 4-2 na Argentina.Mwishoe, walizabwa mabao 2:0 na mabingwa wa Afrika Tunesia.
Tunesia kama mabingwa wa afrika hawakumudu kufika umbali waliofika Sim,ba wa nyika-Kamerun katika Kombe hili mara ilöiopita-yaani finali,hata hivyo, kwa staili yao ya kushambulia, wameacha jina Ujerumani.Wakimudu mpambano wa mwisho dhidi ya Morocco kushinmda, watarudi Ujerumani mwakani kupepea bendera ya Afrika.
Ugiriki imevunja moyo,kwani sio tu haikushinda hata mchezo mmoja,haikutia pia hata bao 1.Kocha wao mjerumani Otto Rehagel,atakua na kazi ngumu kuiongoza Ugiriki katika Kombe la dunia hapa Ujerumani.
Kwa ufupi, Kombe la mashirikisho lililoanza Juni 15 hadi 29, limefungua kweli pazia la Kombe lijalo la dunia.
Ujerumani nayo imejaribu viwanja vyake na kujua dosari za mwisho ziko wapi.Moja kati ya hizo, ziliibuka katika uwanja wa Frankfurt wakati wa finali baina ya Argentina na Brazil pale mvua kali ilionyesha, ilitoboa paa la uwanja na kuvuja.
Ina mwaka mmoja kamati ya maandalio chini ya Beckenbauer,kurekebisha dosari kama hizo ndogo ndogo .Kwa jumla lakini hakuna shaka Ujerumani inayotazamia wageni milioni 1 mwakani,kuukaribisha ulimwengu mikono 2 katika Kombe la dunia.
Kuanzia Juni 9 mwakani, firimbi italia kuanuisha changamoto ya timu 32 kuania FIFA WORLD CUP.Miongoni mwa timu hizo, 5 zitatoka Afrika.Kura timu zitakavyopambana itapigwa desemba mwaka huu mjini Frankfurt baada ya kanda mbali mbali kukamilisha mapambano yao ya kuania tiketi zao za kuja Ujerumani.
Barani Afrika,Kamerun na Afrika Kusini zimo hatarini kupigwa kumbo na kwa mara ya kwanza Black Stars au Ghana ina matumaini.Pamoja nao,Ivory Coast na Angola.Senegal inatiwa shindo kali na chipukizi mwengine-Togo.
Si ajabu kwahivyo, Kombe la dunia 2006 Ujerumani likajionea timu mpya zikipepea bendera ya Afrika katika na sio tu zile za desturi-Kamerun,Morocco,Algeria na Tunesia au hata Senegal.