1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wayatosa maisha baharini

19 Aprili 2016

Kinyang'anyiro cha kuania madaraka Brazil, msiba wa wakimbizi katika bahari ya Mediterenia na chuki za chama "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani "AfD" dhidi ya waislam ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1IYHL
Bunge la Brazil lapiga kura kuruhusu utaratibu wa kupokonywa madaraka rais Dilma RousseffPicha: Reuters/U. Marcelino

Tuanzie lakini Brazilia ambako baada ya bunge kuunga mkono maombi ya upinzani kutaka rais Dilma Roussef apokonywe madaraka yake,sasa ni zamu ya baraza la Senet kutoa uamuzi wa mwisho. Gazeti la " Landeszeitung Lüneburg" linaandika:"Mwanzo kabisa kinyang'anyiro hiki cha kuania madaraka nchini Brazil kinamkumbusha mtu zile filamu za televisheni zinazopendwa sana nchini humo-zinazoonyesha jinsi fitina na hila zinavyotumiwa na watu kuyafikia malengo yao . Kimsingi mengi zaidi yataingia hatarini, sio pekee mustakbal wa Dilma Rousseff: na zaidi kuliko yote ni utulivu wa nchi hiyo inayoinukia. Michuano ya dimba huangaliwa kama "kichocheo " cha malalamiko yanayoendelea tangu miaka mitatu iliyopita-na michezo ya Olympik ya msimu wa kiangazi mwaka huu inaweza kuwa chachu itakayosababisha mripuko. Wale wale wanasiasa waliooza kwa rushwa ndio wanaochochea machafuko ili kumng'owa madarakani rais anaesifiwa kuwa mwaminifu. Kusema kweli nchi hiyo kubwa kabisa inayoinukia-Brazil haihitaji mageuzi katika kasri la rais,bali taifa linaloheshimu sheria. Pindi fitina na hila zikiendelea nchini humo itaibuka hatari ya kuwaona wapinzani wa demokrasia wakijigeuza waokozi.

Wakimbizi wafuate njia hatari zaidi baada ya ile ya Balkan kufungwa

Baada ya kufungwa ile iliyokuwa ikijulikana kama njia ya Balkan,hofu zilizuka wakimbizi wasije wakaitumia njia hatari zaidi na kuzidi kuyatia hatarini maisha yao. Gazeti la "Thüringischen Landeszeitung" linazungumzia msiba wa wakimbizi katika bahari ya Mediterenia."Hivi sasa mpaka watu kutoka Nigeria na Mali wanapanda mashuwa. Na hapo kimoja ni hakika; makubaliano yanayofikiwa ni ya kukata tikiti ya kiyama. Kufungwa njia ya Balkan,ni jaribio lakini kwa vyovyote vile sio ufumbuzi wa mzozo wa wakimbizi. Serikali kuu ya Ujerumani inabidi ijitokeze na msimamo bayana,itangulie mbele na kuzisaidia nchi mfano wa Ugiriki. Kwasababu kila ufumbuzi wa upande mmoja kitaifa utageuka mzigo kwa wale wasiojua la kufanya na ambao matumaini yao ya mwisho ni kukata tikiti kutafuta maisha bora.

AfD wataka misikiti ifungwe Ujerumani

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu malumbano yaliyosababishwa na chama cha "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani"AfD kuhusu uhuru wa kuabudu nchini Ujerumani. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Aibu ni pale AfD wanapojaribu kila mara kuvuruga msingi wa watu kuishi pamoja,kama inavyodhihirika jinsi viongozi wa chama hicho wasivyojali kuchafua mafanikio ambayo waliotutangulia wameypigania kwa karne kadhaa. Na yote hayo kwasababu ya mbinu za kisiasa. Ni dhahir yote hayo yanakifanya chama cha AfD kuwa hatari. Imesalia miezi 17 hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa. Hadi wakati huu kuna mengi zaidi maovu yanayoweza kuchochewa na AfD.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu