Brazil kulinda hadhi , asema nahodha Thiago Silva
12 Julai 2014Ndoto za Brazil kunyakua taji la sita la kombe la dunia , na kwa mara ya kwanza katika ardhi ya nchi hiyo, ilivunjiliwa mbali wakati Ujerumani ilipoirarua timu hiyo kwa mabao 7-1 katika mchezo wa nusu fainali siku ya Jumanne, wakati Wadachi walipata kipigo cha mikwaju ya penalti kutoka kwa mahasimu wakubwa wa Brazil katika Amerika ya kusini Argentina.
Japokuwa nafasi ya tatu itakuwa kifuta machozi kiasi, nahodha wa timu ya Brazil Thiago Silva amesema wachezaji wa kikosi hicho cha "selecao" watajaribu kuinua heshima na hadhi ya taifa hilo ambalo limebakia katika mshtuko mkubwa kutokana na kipigo hicho wasichokilalia.
Heshima na kulipa kisasi
Pia wana nafasi ya kulipiza kisasi dhidi ya Wadachi , ambao waliwang'oa katika robo fainali katika kombe la dunia nchini Afrika kusini miaka minne iliyopita.
"Tuna kiwango cha juu kabisa cha motisha", Thiago Silva , ambaye alikosa kucheza katika mchezo dhidi ya Ujerumani kutokana na kuzuiwa baada ya kuwa ameoneshwa kadi tatu za njano, amewaambia waandishi habari katika uwanja wa taifa mjini Brasilia.
"Ni dhahiri tuna lengo tofauti hivi sasa na hatupambani kuwania nafasi ya kwanza lakini inahusu hadhi yetu na heshima," ameongeza mlinzi huyo wa kati.
"Wakati ukivaa jezi ile iliyo na nyota tano kifuani unapaswa kuiheshimu. Sijalala kwa siku kadhaa nikifikiria kuhusu kombe hili la dunia na juu ya fainali katika uwanja wa Maracana siku ya Jumapili, lakini haijawa hivyo.
Filipe apanga mabadiliko
Lakini Luiz Filipe Scolari amesema anapanga kufanya mabadiliko kidogo kutoka kikosi ambacho kilianza dhidi ya Ujerumani , akiwazawadia wachezaji ambao hawakucheza ama walipata muda mchache uwanjani katika fainali hizi.
Scolari ameungwa mkono na rais mteule wa shirikisho la kandanda la Brazil CBF licha ya kipigo cha kugaragazwa ilichokipata Brazil siku ya Jumanne lakini hakufichua iwapo anapanga kuendelea kuwa kocha wa kikosi hicho ama atajiuzulu baada ya kombe la dunia.
Kocha huyo wa Brazil amekiri kuwa wiki sita zilizopita ambazo zimekuwa zenye kazi ngumu nje na ndani ya uwanja zitaendelea kumfuata katika maisha yake yote.
"Mambo mengi yamebadilika na yameathiri maisha yangu kwa mazuri na mabaya. Katika siku zinazokuja nitajaribu kuendelea na maisha yangu ya kawaida, ambayo nimeyaacha kwa kiasi fulani katika siku za hivi karibuni," amesema Scolari kabla ya mchezo wa leo(12.07.2014) kati ya Brazil na Uholanzi mjini Brasilia.
Kipigo kitamfuata Scolari maisha yake yote
Hata hivyo ameonesha shaka iwapo ataendelea na kazi hiyo ya kukinoa kikosi cha selecao hapo baadaye, baada ya kusema atakumbuka maisha yake yote kipigo hicho cha mabao 7-1 dhidi ya Ujerumani.
"Kazi yangu inamalizika baada ya mchezo wa mwisho wa timu ya taifa, ambayo ni kesho (leo). Baada ya hapo nitaandika ripoti , na kisha rais mpya wa shirikisho la kandanda la Brazil Marco Polo (del Nero) atazungumza na timu yake, wataangalia kile kilichotokea, wataangalia kile nilichokifanya vizuri na vibaya katika kazi yangu," Scolari amesema mjini Brasilia.
Hakuondoa uwezekano wa kuendelea kuifunza timu ya taifa ya Brazil, licha ya kuwa inaripotiwa kuwa si rahisi tena.
Fainali ya kombe la dunia mwaka huu 2014 itafanyika katika uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro kesho Jumapili (13.07.2014), ambapo Ujerumani itaoneshana kazi na Argentina.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Daniel Gakuba