Boubakar Keita aongoza matokeo ya awali Mali
31 Julai 2013Waziri wa mambo ya ndani wa Mali, Kanali Moussa Sinko Coulibaly, amesema jana waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita amewaacha mbali wapinzani wake na kama hali hiyo itaendelea ina maana hakutakuwa na haja ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi. Matokeo hayo yanatokana na thuluthi moja ya kura zote zilizopigwa katika majimbo yote ya uchaguzi nchini kote. Coulibaly alikataa maombi ya waandishi wa habari waliomtaka ataje takwimu kamili na badala yake kusema matokeo hayo yalikuwa yamethibitishwa na tume ya uchaguzi.
Amadou Koita, msemaji wa waziri wa zamani wa fedha, Soumaila Cisse, ambaye Coulibaly anasema anashikilia nafasi ya pili kwa sasa, amelieleza tangazo hilo kuwa kashfa na kuhoji kwa nini waziri huyo alikataa kutoa takwimu kuunga mkono kauli yake. "Tunayakaa matokeo haya yaliyotangazwa na waziri. Tunamtaka ajiuzulu na tume ya kimataifa iundwe ili ihesabu kura," amesema Koita.
Koita pia alihoji vipi waziri angeweza kubashiri matokeo ya mwisho kwa kuzingatia thuluthi moja tu ya kura wakati tume ya uchaguzi iliposema imeshahesabu asilimia 12 ya kura.
Muda mfupi baada ya matokeo hayo ya awali kutangazwa magari na baiskeli zilipiga honi katika barabara za mji mkuu, Bamako, huku wafuasi wa Ibrahim Boubacar Keita wakipiga kelele wakisema "IBK" "IBK" "IBK", kama anavyojulikana na wengi nchini Mali kwa herufi za mwanzo za majina yake matatu.
Upigaji kura wa siku ya Jumapili ulifanyika kwa amani na waangalizi wa uchaguzi huo wameupongeza, lakini hali ya wasiwasi inazidi kuongeza huku matokeo rasmi ya mwisho yakikaribia kutangazwa.
Nigeria kuondoa wanajeshi wake Mali
Wakati hayo yakiendelea, Nigeria imesema itaanza leo kuwaondoa baadhi ya wanajeshi wake 1,200 walioko nchini Mali na kuwarudisha nyumbani kuendelea na kazi yao ya kufanya operesheni za usalama. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya jeshi iliyotolewa jana. Brigedia Jenerali Chris Olukolade wa jeshi la Nigeria amesema katika taarifa hiyo wanajeshi watakaorudi nyumbani ni wale ambao hawakujumishwa katika muundo wa kikosi kipya maalumu cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mali.
Hata hivyo Olukalade hakutaja ni wanajeshi wangapi watakaorudishwa nyumbani, akisema tu kwamba wanajeshi kadhaa pamoja na vifaa, wataendelea kushiriki katika tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Mali, ikiwa ni pamoja na kusimamia shughuli katika hospitali moja inayoendeshwa na Nigeria.
Nigeria imekuwa ikipanga kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Mali kwa kuwa inahitaji wanajeshi wengi zaidi kupambana na upinzani wa wanamgambo wa kiislamu katika ardhi yake.
Mandishi: Josephat Charo/RTRE
Mhariri: Saumu Yusuf