Peter Bosz apigwa kalamu Leverkusen
23 Machi 2021Klabu hiyo imesema nafasi ya Bosz itachukuliwa na Hannes Wolf, mwenye umri wa miaka 39, ambaye amekuwa akiinoa timu ya Ujerumani ya wachezaji wa chini ya miaka 18, atachukua usukani hadi mwisho wa msimu.
Leverkusen ilikuwa moja ya timu kali kwenye ligi ya Bundesliga hadi pale walipotiwa doa na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Bayern Munich mnamo Desemba 19 katika mchezo wa mwisho kabla ya mapumziko ya msimu wa baridi. Soma zaidi Leverkusen vinara wapya wa Bundesliga
Tangu wakati huo, Leverkusen imeshinda mara nne tu katika jumla ya mechi 17 na kupoteza mara 10, pamoja na kutolewa kwenye kinyang'anyiro cha Kombe la Ulaya na kombe la Shirikisho nchini Ujerumani.
Katika mechi yao iliyopita Leverkusen ilicharazwa mabao 3-0 na klabu iliyokuwa katika nafasi ya kushuka daraja, Hertha Berlin. Matokeo haya yameifanya imeteremka hadi nafasi ya 6 wakisajili mwanya wa pointi saba chini ya Eintracht Frankfurt na kuwa timu ya mwisho katika nafasi ya tiketi ya kufuzu kwa ligi ya Champions.
Hakukua na njia mbadala
"Tulifikia uamuzi kwamba kuagana na Peter Bosz hakuwezi kuepukika kwa kuzingatia maendeleo ya wiki zilizopita,
Kupoteza 3-0 kwa Hertha Jumapili kwa bahati mbaya ilikuwa kama tabia. Timu yetu imeangukia katika muundo huo tena na tena. Hatukufanikiwa kurekebisha makosa ya kila wakati na kurudi kwenye mafanikio." alisema Mkurugenzi mtendaji wa Leverkusen Rudi Voller.
Voller amesema Leverkusen itaendelea "kumthamini sana" Bosz, ambaye mwanzoni alichukua madaraka kutoka kwa Heiko Herrlich mnamo Desemba 2018. Msimu uliopita Bosz aliongoza Leverkusen kumaliza katika nafasi ya nne katika ligi ya Bundesliga na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa, kisha kufuzu kwa Ligi ya Ulaya na Fainali ya Kombe la Shirikisho, Bayern Munich iliishinda Leverkusen 4-2 katika fainali. Soma zaidi Bayern na Leverkusen, nani atalitwaa taji la DFB Pokal Jumamosi?
Wolf amevutia wengi
Aidha makocha wasaidizi Hendrie Kruzen na Rob Maas, na Kocha wa mazoezi ya misuli Terry Peters pia wataondoka pamoja na Bosz.
Kocha mpya Hannes Wolf atasaidiwa na Peter Hermann, ambaye anarudi Leverkusen. Hermann mwenye umri wa miaka 69 ana ushirika wa miaka 29 na Leverkusen kama mchezaji, kocha msaidizi na kocha wa muda.
Wolf hapo awali aliongoza Stuttgart kupandishwa daraja katika Bundesliga mnamo 2017, lakini alifutwa kazi msimu uliofuata baada ya matokeo mabaya. Baadaye aliteuliwa na klabu ya zamani ya Bundesliga Hamburger SV lakini haikuweza kupanda daraja.
"Licha ya kuwa kocha mchanga sana, Hannes Wolf amevutia vilabu vikubwa haswa kupitia kuipandisha daraja Stuttgart, Hannes anawakilisha aina ya soka ambayo tunataka kucheza kama Bayer Leverkusen; Kali, ya kushambulia, ya kuvutia. Na, kwa kweli, yenye mafanikio." amesema Mkurugenzi wa michezo wa Leverkusen Simon Rolfes.
Chanzo/APE