Botswana yatoa waranti wa kukamatwa rais wa zamani Ian Khama
30 Desemba 2022Tovuti ya habari ya News24 imeripoti kuwa Khama anakabiliwa na mashtaka 14 ya uhalifu nchini mwake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa jana na tovuti hiyo, mashtaka hayo ni pamoja na kumiliki silaha kinyume cha sheria na utakatishaji wa fedha.
Rais wa zamani wa Botswana aitwa mahakamani
Hata hivyo, Khama amekanusha mashtaka dhidi yake, akiyaita kuwa ya uwongo na yaliyochochewa kisiasa.
Iwapo mahakama itamkuta na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani.
Mwezi Aprili, Khama alikiambia kituo cha habari cha Afrika Kusini, SABC kwamba anajihisi yuko salama akiwa Afrika Kusini na huenda kamwe asirejee Botswana, lakini amekanusha kuukimbia mkono wa sheria.
Khama aliyejiuzulu mwaka 2018 baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 10, alikosana na mrithi wake, Mokgweetsi Masisi, ambaye amemshutumu kwa kutawala kimabavu.