Boris Johnson na Zahma ya Brexit Magazetini
4 Septemba 2019
Tunaanza na mpango wa Uingereza kutaka kujitoa katika Umoja wa ulaya- Brexit. Mbio za waziri mkuu Boris Johnson zinaonyesha zimeishia sakafuni linaandika gazeti la "Mittelbayerische Zeitung": Ishara zinaonyesha uchaguzi wa kabla ya wakati utaitishwa nchini Uingereza na kwa namna hiyo kuzidisha makali ya zahma ya Brexit. Mivutano miongoni mwa vyama vya kisiasa itaongezeka kati ya wale wanaopigania msimamo mkali wa Brexit na wale wanaoelemea upande wa Umoja wa Ulaya. Kampeni za uchaguzi katika nchi ambayo tokea hapo inatokota, inaweza kuzidisha mfarakano. Na inaweza kuwa chanzo- kama ilivyoshuhudiwa mwaka 2017- cha kutopatikana chama chochote kitakachoibuka na wingi wa viti bungeni. Kura ya pili ya maoni ndio ufumbuzi wa maana."
Serikali ya muungano ya mahasimu wawili yatarajiwa Italia
Katika wakati ambapo Uingereza kunatokota, Italia inashusha pumzi. Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linachambua kuhusu uwezekano wa kuundwa serikali nchini humo na kuandika:"Kiongozi wa chama cha Nyota tano Luigi di Maio ameusifu utaratibu wa kuwataka wafuasi wa chama chake watamke kama wanaunga mkono au la kuundwa serikali pamoja na wanasocial Democrat kuwa ni utaratibu wa demokrasia ya moja kwa moja. Si kweli. Haiwezekani linasema gazeti hilo na kutoa sababu likisema vipi wafuasi elfu kadhaa tuu wa Nyota tano wanaweza kuamua hatima ya wataliana milioni 60 tena mtandaoni, uwanja ambao hauna sifa nzuri linapohusika suala la uwazi na uhakika."
CDU na sera ya mabadiliko ya tabianchi
Mada ya tatu magazetini inaturejesha hapa hapa Ujerumani ambako chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU kinajadiliana kuhusu mkondo wanaobidi kufuata katika suala la mabadiliko ya tabianchi. Gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" linaandika:"Haitokuwa rahisi kwa CDU kubadilisha msimamo wake kuelekea suala la mabadiliko ya tabianchi. Kundi linalotetea masilahi ya kiuchumi litaweka vizuwizi, matawi ya chama katika maeneo ya mashariki yana wasi wasi na neno kodi ya moshi unaochafua mazingira linazusha hofu. Mwenyekiti wa chama Kramp-Karrenbauer amelazimika kumuomba Wolfgang Schäuble aingilie kati. Schäuble amezifutilia mbali hofu hizo na kutoa picha ya faida inayoweza kupatikana. Anasema hakuna cha bure katika mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini bila ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kila kitu kitakuwa ghali. CDU wanabidi walizingatie hilo. Wakitaka kung'ang'ania msimamo wao wa zamani kuhusu sera ya mabadailiko ya tabia nchi, basi watambue pia wataipoteza fursa kubwa iliyoko na sio tu kwa chama chao.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspress
Mhariri:Yusuf Saumu