1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bomu laua watu kadhaa Istanbul

7 Juni 2016

Watu 11 wameuawa na wengine wapatao 36 wamejeruhiwa baada ya bomu la kutegwa kwenye gari kulipuka Istanbul, Uturuki. Bomu liliwalenga polisi na lililipuka wakati watu wengi walikuwa wakielekea kazini.

https://p.dw.com/p/1J1nR
Gari la polisi lililoshambuliwa na bomu Istanbul
Picha: Reuters/O. Orsal

Magari ya kusafirisha wagonjwa yaliendeshwa kwa kasi katika mitaa ya Istanbul kuchukua waliojeruhiwa katika mlipuko wa bomu. Bomu hilo lililokuwa limetegwa kwenye gari lililipuka pale ambapo mabasi ya polisi yalipopita karibu nalo. Mlipuko uliharibu pia majengo na magari mengine yaliyokuwa karibu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amelaani shambulio hilo akisema washambuliaji wana roho ngumu kulipua mabomu wakati wa Ramadhani.

Akitoa maelezo zaidi kuhusu mlipuko, Gavana wa Istanbul, Vasip Sahin amesema: "Bomu la kutegwa garini lililipua magari yaliyokuwa yakibeba polisi wetu wa kikosi maalumu na yalipokuwa yakipita barabarani saa mbili na dakika arobaini asubuhi. Bomu limesababisha vifo vya polisi saba na raia wa kawaida wanne. Mungu azirehemu roho zao. Watu 36 wamejeruhiwa. Upelelezi unaendelea."

Historia ndefu ya vita na PKK

Istanbul ndio jiji kubwa zaidi nchini Uturuki na hii ni mara ya nne kwa jiji hilo kushuhudia shambulio kubwa la bomu ndani ya mwaka huu. Bado hakuna kundi lililokiri kuhusika na shambulio la Jumanne lakini wanamgambo wa chama cha Kikurdi cha PKK kilichopigwa marufuku, wamekuwa wakifanya mashambulio kama hayo katika siku za nyuma, likiwemo shambulio moja hapo hapo Istanbul mwezi uliopita.

Gari la polisi lililoshambuliwa na bomu Istanbul
Gari la polisi lililoshambuliwa na bomu IstanbulPicha: Reuters/O. Orsal

Chama cha PKK ambacho kiko kwenye mgogoro na serikali ya Uturuki tangu mwaka 1984, mara kwa mara wapiganaji wake wamekuwa wakishambulia magari ya polisi na ya jeshi kwa kulipua mabomu ya kwenye magari.

Pamoja na hayo, wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu wamelaumiwa kwa kulipua mabomu kadhaa Uturuki. Inakadiriwa kwamba maafisa wa usalama wapatao 500 wa Uturuki wameuliwa katika mashambulio kama hayo au katika mapambano na wanamgambo wa Kikurdi. Kwa upande mwingine, jeshi la Uturuki linadai kuwa limefanikiwa kuwaua wapiganaji wa PKK wapatao 5,000 katika operesheni zinazoendeshwa Uturuki kwenyewe na Iraq ya Kaskazini ambapo PKK ina ngome kubwa.

PKK inataka Wakurdi wanaoishi Kusini Mashariki mwa Uturuki waweze kujitawala wenyewe. Mapigano kati ya majeshi ya serikali na chama hicho yamekuwa yakiendelea kwa miongo kadhaa na mpaka sasa yamesababisha vifo vya watu wapatao 40,000.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/AP

Mhariri: Saumu Yusuf