Bomu lasababisha vifo vya watu zaidi ya 20 Nigeria
26 Juni 2014Mji huo kwa hivi sasa unakabiliwa na kitisho chamashambulizi ya kundi la kiislamu lenye itikadi kali la Boko Haram.
Shirika la Nigeria la kukabiliana na majanga ya dharura(MENA) limesema mkasa huo umetokea jana jioni ikiwa saa moja kabla ya mechi ya kombe la dunia iliyokuwa ikiikutanisha Nigeria na Argentina. Wakati mkasa huo ukitokea katika jengo hilo lenye maduka mengi linaloitwa "Emab Plaza" ampapo idadi kubwa ya watu ilikuwa katika pirikapirika za kunuanua bidhaa mbalimbali.
Mwanamke mmoja aliyeshuhudia mkasa huyo alikuwa na haya ya kusema "Kwa wakati huo tulikuwa ndani ya duka nikiwa na bosi wangu tukinunua vitu, hatua fupi kutoka tulipokuwa tulisika mripuko. Kulikuwa na gari imeegeshwa nje kwa hivyo nina amini bomu hilo lilitegwa ndani ya gari"
Kauli ya polisi baada ya tukio
Frank Mba, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Nigeria alisema kwa wakati huo idadi ya watu waliokufa ilifikia 21 na waliojeruhiwa 17. Aidha amesema watu wawili wanaohusika wametiwa mbaroni. "Kwa wakati huu hatuwezi kuzungumza zaidi, hatuwezi kukueleza chanzo au aina ya mripuko ambao umetumika, hatuwezi kukupa pia idadi kamili ya watu waliokufa na kujeruhiwa. Hatuwezi kukupa taarifa zaidi "
Afisa huyo wa polisi pamoja na kutahadharisha umma kutokuwa karibu na eneo la mripuko kwa lengo la kuepusha athari nyingine zinazoweza kutokea katika eneo hilo amesema kwa hivi sasa bado wapo katika hatua za awali na za msingi za uchunguzi kufuatia tukio hilo ambapo baadae watatoa taarifa zaidi. Lakini baadae idara ya habari ya taifa ilisema ilisema mtu wa pili aliyehusika na tukio hilo alipigwa risasi na polisi pale alipojaribu kutoroka na akiwa na pikipiki.
Msemaji mwandamizi wa serikali ya Nigeria Mike Omeri alithibitisha kuwa mrupoko huo unatokana na bomu. Na msemaji wa shirika la uokozi MENA, Manzo Ezekiel aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa timu ya waokozi ilipelekwa katika eneo la tukio kwa ajili ya shughuli hiyo.
Mtu mwingine aliyeshuhudia mkasa huo amenukuliwa akisema "Katika hali kama hii viongozi hawawezi kutuambia hawaelewi kinchoendelea,tuna vikosi vya usalama,hakuna mtu aliye juu ya serikali,hakuna mwenye nguvu zaidi ya serikali, serikali ina nguvu, serikali ina kila kitu. Kwa hivyo wanawajibu, wanapaswa kutatua matatizo. Na wanapaswa kutuarifu kipi kimekosewa na kipi sahihi."
Mripuko ulitokea wakati wa pirika nyingi za kibiashara na kwamba takribani magari 40 yameharibika vibaya.
Kundi la Boko Haram ambalo limekuwa likipigiwa kelele duniani kote kutokana na kuwaateka wasichana 200 mwezi Aprili limewahi kuishambilia Nigeria mara mbili katika kipindi kisichozidi wiki 10 zilizopita. Moja kati ya mkasa wa kukumbukwa ni pamoja na mripuko wa Aprili 14 uliosababisha vifo vya watu 75 katika kituo cha usafiri cha Nyanya mjini Abuja.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman