Bomba la mafuta la Saudi Arabia lashambuliwa
14 Mei 2019Siku chache baada ya Marekani kupeleka ndege za kivita na meli ya mashambulizi kuimarisha meli yake ya ubabeaji ndege iliyoko katika kanda hiyo, Saudi Arabia, ambayo ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa mauzo ya mafuta imesema vituo viwili vya kuchimba mafuta vimelengwa katika mashambulizi ya leo.
Tangazo hilo limekuja saa kadhaa baada ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen kusema wamelenga miundombinu muhimu nchini Saudi Arabia, ambayo inaongoza muungano wa kijeshi dhidi yao.
Waziri wa nishati wa Saudi Arabia Khalid al-Falih amesema shirika la uw la Saudi Arabia Aramco, limelifunga kwa muda bomba hilo ili kutathmini hali yake, lakini akaongeza kuwa uzalishaji na mauzo ya mafuta havijatatizwa. Vituo hivyo vilivyoshambuliwa viko magharibi mwa mji mkuu Riyadh, katika maeneo ya Daadmi na Afeef.
Falih amesema tukio hilo lilikuwa kitendo cha kigaidi, ambacho siyo tu kinalenga falme hiyo lakini pia usalama wa ugavi wa mafuta kwa dunia pamoja na uchumi wa dunia.
Wahouthi wadai kulipa kisasi
Msemaji wa Wahouthi Mohammed Abdusalam aliandika kwenye ukurasa wa Twitter kwamba mashambulizi hayo yalikuwa jibu kwa wavamizi wanaoendelea kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Yemen.
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu waliingilia katika vita nchini Yemen kuisaidia serikali ya rais Abdul-Rabb Hadi inayotambulika kimataifa, dhidi ya Wahouthi Machi 2015.
Bomba hilo lililoshambuliwa lwenye urefu wa kilomita 1,200 linahudumu kama mbadala kwa usafirishaji wa mafuta ghafi ya Saudi Arabia iwapo ujia wenye umuhimu wa kimkakati wa Hormuz ukatoke kufungwa.
Iran imetishia mara kadhaa kuufunga ujia huo ikiwa kutatokea makabiliano ya kijeshi na Marekani. Mashambulizi dhidi ya bomba hilo yamekuja baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu kusema meli nne ziliharibiwa katika mashambulizi ya hujuma nje ya falme ya Fujairah, karibu na Hormuz siku ya Jumapili.
Chanzo: Mashirika.