Boksiti ya Guinea- Conakry
Hakuna nchi yenye utajiri wa madini ya boksiti kama nchi ndogo ya Afrika magharibi ya Guinea. Mali ghafi hiyo inachimbwa kutoka mgodi wa Débélé ulioko katika jimbo la magharibi la Kindia.
Kupata malighafi kwa njia ya mripuko
Takriban kunakuwa na miripuko miwili kwa siku katika mgodi wa Débélé nchini Guinea. Mfanyakazi huripua kwa baruti majabali yalioko migodini yanayoundwa na mali ghafi muhimu ya madini ya boksiti kwa ajili ya kuzalisha aluminiamu.
Uchimbaji kwa utaratibu wa asili
Baada ya kuondolewa kwa moshi, boksiti huhamishiwa mahala pengine. Utaratibu huo umekuwa ukitumika kwa miongo kadhaa: Magari ya kuchimba hupakia mapande ya jabali kwenye malori na kuyapeleka kwenye kiwanda kilioko karibu ambako huvunjwa na kuwa vipande vidogo. Mchakato huo ni mgumu na unachukuwa muda.
Magari ya uchimbaji badala ya wafanyakazi
Kazi hufanyika kwa urahisi zaidi. Magari hayo hufanya kazi nyingi zaidi kwa wakati huo huo. Yanachimba majabali yenye boksiti yalioko ardhini, yanayavunja ili kuwa madogo na yanayatia kwenye malori. Vyama vya wafanyakazi vinashutumu kwamba gari hilo moja la kuchimba linachukuwa nafasi ya wafanyakazi 300.
Wataalamu wa ufundi
Magari hayo ya kuchimba yamenunuliwa kutoka kampuni ya Ujerumani na mwendeshaji mgodi huo kampuni ya Rusal ya Urusi. Iwapo mashine huharibika analetwa mhandisi mkuu na timu yake ambao wamepatiwa mafunzo Ujerumani kuyakarabati magari hayo maalum.
Kanda yenye utajiri wa mali ghafi
Uvunjaji wa majabali na ukanda wa migodi uko katika mji wa Débélé katika jimbo la Kindia. Tokea mwaka 1972 boksiti imekuwa ikichimbwa katika jimbo hili la magharibi mwa nchi. Watu wa hapo wanaishi na migodi na kutokana na migodi.
Chini ya mikono ya Urusi
Warusi walikuwa tayari wako katika nchi hiyo zaidi ya miaka 20 iliopita. Kwa hivi sasa kampuni hiyo ya Moscow ya Rusal inashughulikia mgodi wa Débélé. Takriban watu 1,200 wanafanya kazi hapo na wengi wanaishi Kindia mji ulioko kama kilomita 50.
Nchi ndogo na akiba kubwa
Inakadiriwa kwamba ina akiba ya boksiti ya tani bilioni 10 na hakuna nchi duniani yenye utajiri wa madini hayo kama nchi hiyo ndogo ya Afrika magharibi Guinea. Nchi hiyo inasafirisha kwa wingi madini hayo na kuijaza hazina ya taifa.
Wananchi wanaendelea kuwa maskini
Sehemu kubwa ya wananchi wanaishi kwa kutegemea pungufu ya dola moja kwa siku. Nchi za nje ndio zenye kufaidika na uzalishaji wa aluminiamu: kwa sababu ya rushwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa Guinea imeshindwa kuwa na viwanda vyake yenyewe ambapo ingeliweza kushughulikia uzalishaji wa aluminiamu kutokana na madini ya boksiti.
Lengo ni Ukraine
Mwisho wa siku katika mgodi wa Débélé, boksiti inakuwa tayari kusafirishwa. Kampuni ya Rusal inazalisha hadi tani bilioni 3.5 ya ardhi yenye thamani kwa mwaka. Madini hayo huendelea kufanyiwa kazi zaidi hususan nchini Ukraine. Kwa kutumia nishati kubwa aluminiamu huzalishwa kutokana na mali ghafi hiyo.
Tegemezi kwa soko la dunia
Boksiti hupelekwa kwa treni hadi bandari ya mji mkuu Conakry na kutoka hapo husafirishwa kwa meli. Tani tano za boksiti zinaweza kuzalisha tani moja ya aluminiamu ambapo thamani yake katika soko la dunia ni dola 2,000 ingawa kwa hivi sasa bei zinashuka.