Boko Haram yawaachia wasichana iliowateka
21 Machi 2018Wapiganaji hao waliingia katika mji wa Dapchi majira ya saa nane alfajiri wakiwa kwenye jumla ya magari tisa na wasichana hao waliachwa katikati mwa mji. Wakazi wa eneo hilo walioshikwa na taharuki walijitokeza kutoka majumbani, na kuwasikia wanamgambo wakisema, "hili ni onyo kwenu nyote, tumefanya hivi kwa huruma, msirudie kuwapeleka wasichana hawa mashuleni". Boko Haram inamaanisha "Elimu ya nchi za Magharibi hairuhusiwi" kwa lugha ya Kihaussa.
Serikali ya Nigeria imesema wasichana 101 kati ya 110 wamethibitishwa kuachiwa na kwamba idadi nyingine itatolewa baada ya wasichana waliobaki nao kurejeshwa. Waziri wa habari Lai Mohammed amesema katika taarifa yake kwamba, "hapakuwa na fidia yoyote iliyolipwa", akiongeza kuwa wasichana wameachiwa "kupitia juhudi za mgongo wa nyuma na usaidizi wa baadhi ya marafiki wa nchi, na hapakuwa na masharti". Zaidi Lai anasema kuwa "hadi sasa nathibitisha jumla ya wasichana 91 na mvulana mmoja wameachiwa. idadi inazidi kuongezeka, wasichana wengi ambao wameachiwa hawakushushwa sehemu moja. Walishushwa tu barabarni na wakaenda nyumbani kwa wazazi wao. Sasa wanaombwa kuja kuandikishwa kwenye vituo."
Utekaji nyara huo mkubwa na namna serikali ilivyoushughulikia ulirejesha kumbukumbu za kuumiza za shambulio la mwaka 2014 katika shule ya bweni ya Chibok. Wanamgambo wa Boko Haram waliwateka wasichana 276 na 100 kati yao hawakurejea nyumbani kamwe. Baadhi ya wasichana walilazimishwa kuolewa na watekaji na wengi wao wamezalishwa watoto na wanamgambo hao.
Utekaji wa karibuni unadhaniwa kutekelezwa na kundi lililogawika kutoka Boko Haram linalofungamana na Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, ambalo limemkosoa kiongozi wa Boko Haram kwa kuwalenga raia na badala yake kulilenga jeshi na mataifa ya magharibi.
Wakazi wa Dapchi waliondoka asubuhi ya Jumatano mara baada ya kusikia taarifa kwamba magari ya Boko Haram yanaelekea katikati mwa mji. Umar Hassan ameieleza AFP kwamba walijongea eneo hilo lakini kwa kujificha na kwa mbali waliwaona mabinti zao wakiteremka kutoka kwenye magari. Mkazi mwingine Kachallah Musa naye anasimulia akisema, " waliwakusanya wasichana na kuzungumza nao kwa dakika chache na kuondoka bila ya kufanya vurugu yoyote".
Wasichana hao wamepelekwa katika hospitali kuu ya Dapchi na wanapatiwa nasaha na washauri kwa mujibu wa waziri wa habari. Kuachiwa kwa wasichana hao kunakuja siku moja baada ya shirika la haki za binadamu la Amnesty International kulituhumu jeshi la Nigeria kwa kushindwa kushughulikia onyo lililotolewa juu ya shambulio hilo mwezi uliopita. Jeshi limeiita ripoti hiyo kuwa ni "uongo wa wazi". Waziri wa ulinzi wa Nigeria Brigedia Jenerali Mansur Dan Ali amenukuliwa akisema "kimsingi nataka kuelezea dhana iliyokuwepo kwamba wasichana hawa wasingeachiwa. Mtakumbuka mazungumzo ya mwisho tuliyokuwa nayo, nilisema kwamba miezi miwili au chini ya hapo, tungeweza kuwapata. Kwa hiyo hizi ni juhudi za rais na msaada aliotupatia na matokeo yamejionyesha sasa."
Serikali ya Nigeria imesherehekea kuachiwa kwa wasichana hao, msaidizi wa rais Bashir Ahamad ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa "habari njema kutoka dapchi, jimbo la Yobo. Asante Mungu kwa kuwarejesha salama dada zetu, Alhamdulillah".
Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Josephat Charo