Boko Haram yauwa wanajeshi watatu wa Nigeria
29 Novemba 2018Wapiganaji wa kundi la Boko Haram wamewauwa wanajeshi watatu katika shambulio dhidi ya kituo cha jeshi kaskazini mashariki mwa jimbo la Nigeria la Borno karibu na Ziwa Chad, duru za kijeshi na raia zimesema.
Wapiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu la Afrika Magharibi wakiwa na magari kadhaa walishambulia kituo hicho cha jeshi katika kijiji cha Cross-Kauwa siku ya Jumanne na kupambana na majeshi katika mapambano ya saa nzima.
Afisa mmoja wa jeshi amesema wanajeshi walipambana na wapiganaji hao lakini walielemewa na walilazimika kujiondoa kutoka katika kituo hicho.
Tangu Julai shirika la AFP limeorodhesha mashambulizi 17 katika vituo vya kijeshi, ambapo mengi yao yamedaiwa kufanywa na kundi hilo lijiitalo Dola la Kiislamu la Afrika Magharibi.