1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

220814 Nigeria Boko Haram

Josephat Nyiro Charo26 Agosti 2014

Mapambano ya kutaka kuwakomboa wasichana wa shule waliotekwa na Boko Haram yanaendelea sambamba na mapambano dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Nigeria. Serikali inakabiliwa na shinikizo.

https://p.dw.com/p/1D1In
Anschlag auf ein Hotel in Bauchi Nigeria
Shambulizi la Boko Haram katika hoteli moja mjini BauchiPicha: picture-alliance/dpa

Ugonjwa hatari wa Ebola ni suala linalozungumziwa sana nchini Nigeria wakati huu. Ugonjwa huo unayahatarisha maisha ya wasichana wa shule waliotekwa nyara katika kijiji cha Chibok na wanaoendelea kuzuiliwa na wanamgambo wa kundi la wanaitikadi kali la Boko Haram.

Hawatachoka. Wanaharakati wa kampeni ya kutaka wasichana hao waachiwe huru na warejeshwe makwao, BringBackOurGirls, mjini Abuja. Kwa zaidi ya siku 130 wasichana hao wamekuwa mikononi mwa wanamgambo wa Boko Haram. Baadhi walifaulu kukimbia, lakini wasichana wapatao 220 bado hawajulikani waliko.

Taarifa za kutekwa wasichana hao ziligonga vichwa vya habari na kuzungumziwa sana, lakini sasa inaonekana hakuna anayetaka kusikia kuhusu wasichana hao. Hata katika ofisi za shirika la Unity Fountains katikati mwa Abuja ambako kundi la wanaharakati hao hukutana mara kwa mara, kumekuwa na kimya kuhusu wasichana hao.

Wakili wao Maryam Uwais ameeleza kwa nini. "Mambo yanatokea Nigeria kila uchao. Kuna matatizo mengi yanayojitokeza. Sasa ni ugonjwa wa Ebola unaogonga vichwa vya habari. Ndio maana tumejitahidi sana kuendelea na mikutano yetu kuendelea kuyazungumzia mambo haya."

Machafuko yaendelea bila kikomo

Jambo lililo wazi ni kwamba machafuko kaskazini mwa Nigeria yanaendelea bila jitihada zozote za kuyakomesha na wanamgambo wa Boko Haram wanaendelea kuyadhibiti maeneo zaidi. Alhamisi iliyopita wanamgambo hao waliiteka miji katika majimbo ya Borno na Yobe. Wiki iliyopita vijana kadhaa walitekwa nyara wakati vijiji vilipovamiwa. Vijana hao watafundishwa kuwa wapiganaji lakini pia watadhalilishwa kingono.

Wohnhaus in den Gwoza-Bergen
Makazi katika milima ya GwozaPicha: privat

Watu wanaominiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram wanakidhibiti chuo cha mafunzo cha polisi katika mji wa Gwoza jimboni Borno. Mji huo umekabiliwa na mashambulizi ya wanamambo wa kiislamu. Kwa sasa mji huo unasemekana uko mikononi mwao, lakini mji wa Gwoza si mji pekee unaodhibitiwa na Boko Haram.

Makmid Kamara, mtaalamu wa masuala ya Nigeria katika shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, alisema, "Hali inazidi kuwa mbaya kwa watu wanaoishi maeneo ya vijijini kaskazini mwa Nigeria, hususan jimbo la Borno. Wengi wamenasa kwenye machafuko, wengi wameuwawa na wapiganaji wa Boko Haram na watu wengi wanauwawa pia na vikosi vya usalama vya Nigeria."

Hofu na hali ya kupoteza imani

Kwa maana hiyo hali ya kukosa imani imetanda miongoni mwa raia. Wana hofu kubwa sio tu kwa sababu ya Boko Haram, bali pia wanaliogopa jeshi na kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi. Idayat Hassan, Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo na Demokrasia, CDD, mjini Abuja, alieleza kwa nini. "Kitu ambacho vikosi vya usalama vya Nigeria vimeshindwa kukifanya ni kuzibadili fikra za watu na kupata uungwaji mkono wa raia. Na mpaka hili litakapofanyika, haitawezekana kabisa kuukomesha uasi wa Boko Haram. Hili si tatizo litakalosuhishwa kijeshi."

Goodluck Jonathan spricht mit entkommenen Geiseln
Rais Jonathan alipokutana na wasichana walioponyokaPicha: Wole Emmanuel/AFP/Getty Images

Ukweli uliopo ni kwamba wanajeshi wengi hawaamini suluhisho la kijeshi ndilo litakaloliangamiza kundi la Boko Haram. Mara kwa mara ripoti zinaibuka za wanajeshi kuliasi jeshi la Nigeria. Wake wao walifanya maandamano mnamo Agosti 11 mjini Maiduguri na kuukosoa utawala mzima wa jeshi la nchi hiyo kwa sababu waume wao hawana silaha zinazofaa kukabiliana na magaidi.

Wanasiasa wengi hawalizungumzii suala hili wakati huu. Badala yake tayari wameanza kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanywa Februari mwakani. Kwa siku kadhaa sasa makundi mengi yamekuwa yakifanya kampeni kuwashawishi watu wampigie kura rais wa sasa Goodluck Jonathan. Serikali ya Nigeria imekosolewa na viongozi wa vyama vya upinzani kwa kutochukua hatua madhubuti za kutosha kukabiliana na kundi la Boko Haram.

Mwandishi: Josephat Charo/Gänsler, Katrin

Mhariri:Yusuf Saumu