Boko Haram tishio Afrika magharibi na kati
17 Mei 2014Akizungumza katika mkutano wa kilele mjini Paris Jumamosi (17.05.2014)uliohudhuriwa na viongozi wa Nigeria, Chad, Niger, Cameroon na Benin pamoja na wawakilishi wa Marekani na Uingereza, Hollande amekaririwa akisema " Boko Haram ni tishio kubwa kwa Afrika magharibi nzima na sasa Afrika ya kati ambapo imethibitishwa kuwa na mahusiano na kundi la AQIM (kitengo cha Al Qaeda katika kanda ya Kiislamu ya Maghreb kaskazani mwa Afrika) na makundi mengine ya kigaidi".
Amesema kunahitajika kuanzishwa kwa haraka mpango kabambe wa kubadilishana taarifa na kulinda mipaka.
Rais Goodluck Jonathan ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kufuatia mkutano huo wa kilele kwamba kundi la Boko Haram sio tena tishio la ndani ya nchi hiyo bali limekuwa Al Qaeda ya Afrika magharibi ambapo ni jambo la wazi limekuwa likiendesha harakati zake kama kitengo cha Al Qaeda na kwamba limekuwa kundi la Al Qaeda la Afrika magharibi.
Kuwatokomeza magaidi
Jonathan amesema wameyakinisha kujitolea kwao kulishughilikia suala hilo kikanda, ambapo bila ya ushirikiano wa nchi za Afrika magharibi hawatoweza kuwatokomeza magaidi hao.
Jonathan pia amesema wamejitolea kikamilifu kuwatafuta wasichana zaidi ya 200 waliotekwa na Boko Haram popote pale walipo.
Rais Idriss Deby wa Chad naye amesema nchi jirani na Nigeria ziko tayari kuendesha vita dhidi ya kundi hilo la itikadi kali za Kiislamu kutokana na kuongezeka kwa hofu kwamba litazagaa hadi nchi nyengine na kuliyumbisha eneo zima la Afrika magharibi.Deby amesema "Kuna azma ya kukabiliana na hali hii moja kwa moja .....kuanzisha vita,vita kamili dhidi ya Boko Haram."
Mkutano huo wa Kilele umefanyika ikiwa ni saa chache baada ya shambulio jengine katika eneo la ngome kuu ya kundi la Boko Haram, ambapo maafisa wa mataifa ya magharibi wanataraji utafaulu kuratibu hatua za kuchukuwa dhidi ya kundi hilo la itadi kali za Kiislamu.
Wanamgambo hao ambao wanadai kwamba wanapigana vita takatifu nchini Nigeria huwa wanaweza kutanga tanga na kuingia hadi Cameroon wakiwa huru kabisa ambapo kampuni ya Kichina ilikuja kushambuliwa hapo Ijumaa usiku wa manane.
Mkakati wa pamoja
Maafisa wa Marekani na Uingereza wanataraji kuratibu mkakati na kushirikiana taarifa za kijasusi kugunduwa mahala walipo wasichana wa shule wa Nigeria waliotekwa nyara.
Boko Haram imependekeza kubadilishana wasichana hao 276 ambao inaendelea kuwashikilia na waasi wenzao walioko gerezani venginevyo wametishia kuwauza wasichana hao kwa kuwatumbukiza kwenye utumwa.
Maafisa wamesema hakutakuwepo na operesheni ya kijeshi ya mataifa magharibi kuwakombowa wasichana hao. Maafisa wa serikali ya Uingereza wamesema Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambaye amekubali shingo upande msaada wa kukabiliana na kundi hilo kutoka nje amefuta uwezekano wa kubadilishana wasichana hao na wafungwa.
Hapo Ijumaa Jonathan alifuta ziara yake kwa mji ambako ndiko walikonyakuliwa wasichana hao kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni wasi wasi wa usalama.
Dalili zimezidi kuongezeka kwamba jeshi linakaribia kuasi likilalamika kwamba limezidiwa nguvu na kuelemewa na waasi wa kundi la Boko Haram. Wanajeshi wameliambia shirika la habari la AP kwamba kuna hata baadhi ya wanajeshi wenzao wanaopigana kwa upande wa kundi hilo.Mwaka jana Rais Jonathan alisema anashuku kwamba wanachama na wafuasi wa Boko Haram wamejipenyeza katika kila ngazi ya serikali yake na jeshi likiwemo baraza la mawaziri.
Jambo hilo linakwamisha juhudi za kushirikiana taarifa za kijasusi. Marekani,Ufaransa na Uingereza zote zimetuma wataalamu nchini Nigeria kusaidia kuwatafuta wasichana hao lakini maafisa wa Ufaransa na Marekani wameelezea wasi wasi wao juu ya namna taarifa hizo zitakavyotumiwa.
Boko Haram lajitanafasi kaskazini-mashariki
Eneo la kaskazini-mashariki la Nigeria kwa miaka mitano limekuwa likikabiliwa na ongezeko la mashambulizi ya Boko Haram yanayosababisha maafa.Maelfu ya watu wameuwawa katika mashambulizi hayo wakiwemo raia 1,500 waliouwawa mwaka huu pekee.
Maafisa wa Ufaransa wamesema Cameroon ambayo inapakana na na eneo hilo imeanza kulipa uzito zaidi tatizo hilo baada ya kulipuuza kwa muda mrefu kwa kuliona kuwa ni tatizo la Nigeria. Rais Paul Biya wa Cameroon akizungumza katika mkutano wa kilele wa Paris amesema wako hapo kutangaza vita dhidi ya Boko Haram.
Vyombo vya habari vya China vimeripoti kwamba raia wake mmoja ameuwawa na watu wengine 10 hawajulikani walipo kufuatia shambulio la Ijumaa usiku katika kambi moja kwenye eneo ambako Boko Haram huko nyuma iliwateka nyara raia wa kigeni ikiwemo familia moja ya Ufaransa ya watu saba na mchungaji mmoja.
China ni muwekezaji mkubwa nchini Nigeria ikisaidia kujenga miundo mbinu,miradi ya afya ya taifa na vituo vya michezo na inaagizia mafuta ghafi,mbao na pamba kutoka Nigeria.
Maafisa wanataraji mkutano huo wa kilele wa Jumamosi mjini Paris utashinikiza kuwepo kwa msimamo zaidi wa kimataifa kukabiliana na kundi la Boko Haram.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP/Reuters
Mhariri : Caro Robi