Boko Haram ina kiongozi mpya
4 Agosti 2016Kulingana na jarida la kijihadi la Al Naba, Abu Musab al Barnawi ndiye kiongozi mpya wa Boko Haram aliyepewa wadhifa wa Gavana wa jimbo la magharibi mwa Afrika wa Dola la kiislamu.
Kulingana na mahojiano yaliyochapishwa na IS hapo jana, al Barnawi ambaye tangu mwezi Machi mwaka jana amekuwa msemaji wa Boko Haram amesema atasitisha mashambulizi yanayolenga misikiti na masoko ya waislamu na kudai kuna njama kutoka kwa nchi za magharibi kuigeuza kanda ya kaskazini mwa Nigeria kuwa eneo la kikiristo.
Mahojiano hayo ya Al Barnawi yanaashira kubadilika kwa mkakati wa mashambulizi yanayofanywa na Boko Haram ambao wamewauwa Waislamu wengi zaidi kuliko Wakristo nchini Nigeria kwa kuishambulia misikiti, vijiji na masoko.
Boko Haram inayomaanisha elimu ya magharibi ni haram imekuwa ikizilenga pia shule kwa mashambulizi ya mabomu na kuwateka nyara watoto mashuleni.
Kiongozi huyo mpya wa Boko Haram hasa ameyashutumu mashirika ya kutoa misaada kwa kutumia hali ya ghasia kuwapa waathiriwa vyakula na makaazi na kisha kuwashawishi kubadili dini kutoka Uislamu hadi Ukristo.
Hatma ya Abubakar Shekau ambaye amekuwa kiongozi wa kundi la Boko Haram tangu mwaka 2009 haijulikani. Shekau alionekana mara ya mwisho mwezi machi katika video akionekana mnyonge na kusema mwisho wake umefika.
Kumekuwa na fununu katika wiki za hivi karibuni kuwa Shekau aliyejeruhiwa tumboni, amepokonya wadhifa wa kuwa kiongozi wa Boko haram.
Yuko wapi Shekau?
Mchambuzi wa masuala ya kiusalama Ryan Cummings amesema inaashira kuwa kuna mapinduzi ya uongozi ndani ya Boko Haram dhidi ya Shekau na kundi hilo linafuata mkumbo wa makundi mengine yanayojitenga na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na kujiunga na IS na kuongeza serikali ya Nigeria itakuwa na kibarua cha kutathmini na kukabiliana na kundi ambalo limebadilisha mkakati wake.
Tangu kuingia madarakani mwaka jana, Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameapa kulitokomeza kundi hilo la waasi. Operesheni kabambe za kijeshi zimefanywa dhidi yao ambapo mamia ya watu waliokuwa wameshikwa mateka wameokolewa na kundi hilo licha ya kuwa halijatokomezwa, limesambaratika.
Chini ya uongozi wa Shekau kwa miaka saba iliyopita kundi hilo limefanya uasi mkubwa Kaskazini mwa Nigeria na kusambaa hadi katika nchi jirani na Nigeria kama Niger, Chad na Cameroon.
Mashambulizi ya waasi hao yamesababisha vifo vya watu 20,000 na kuwalaazimisha wengine milioni 2.6 kuyahama makaazi yao, hali ambayo wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu wameitaja kuwa ni janga.
Mwandishi: Caro Robi/afp/ap
Mhariri: Iddi Ssessanga