Boateng aelekea PSG?
25 Julai 2018Mwenyekiti wa miamba hao Karl-Heinz Rummenigge amedokeza leo kuwa mpaka sasa hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya vilabu hivyo viwili, lakini kuna mawasiliano kati ya mawakala wa Boateng.
Akizungumza mjini Philadelphia, Marekani ambako Bayern wanafanya ziara ya kabla ya kuanza msimu mpya, Rummenigge amesema saa ni wakati wa kusubiri na kuona kama watafikia makubaliano ya uhamisho wa mchezaji huyo kwa malipo yatakayokubalika na pande zote.
Kwa mujibu wa jarida la michezo la Ujerumani – Bild, kocha wa PSG Thomas Tuchel aliripotiwa kukutana na Boateng kabla ya Kombe la Dunia mwezi Mei. Hata hivyo, rais wa Bayern Uli Hoeness alisema hakuna ombi rasmi lililotolewa.
Boateng, ambaye alishinda Kombe la Dunia la 2014 na timu ya taifa ya Ujerumani, kwa sasa anakisiwa kugharimu euro milioni 45.5. alikuwa na wakati mgumu katika Kombe la Dunia nchini Urusi baada ya kutimuliwa uwanjani kwa kupewa kadi mbili za njano katika ushindi wa dakika ya mwisho wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Sweden na hivyo kukosa mechi waliyoondolewa katika dimba hilo na Korea Kusini kwa mabao mawili kwa sifuri.
Hata hivyo, beki huyo amedokeza kuhusu nia yake ya kuondoka Bayern, ambao wanaripotiwa kumuwinda Benjamin Pavard, kutoka VfB Stuttgart ambaye alishinda Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Ufaransa na ambaye anaweza kucheza kama beki wa kulia au beki wa katikati.
"Kimsingi, tuna wachezaji wengi katika nafasi hiyo, katika ubora na idadi,” amesema Rummenigge, kuhusiana na Boateng, na mabeki wa kati Mats Hummels na Niklaas Suele ambao wote wako katika kikosi cha taifa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu