1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken kufanya ziara Mashariki ya Kati

4 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kuelekea Mashariki ya Kati katika juhudi za kidiplomasia katikati ya wasiwasi kwamba mzozo kati ya Israel na Hamas unaweza kutanuka zaidi na kuwa wa kikanda.

https://p.dw.com/p/4aqtb
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: ROBERTO SCHMIDT/AFP

Ziara ya Blinken inafanyika baada ya viongozi kadhaa wa Iran kuapa kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na shambulio lililofanyika jana karibu na kaburi la jenerali wa kijeshi wa Iran, Qassem Soleiman wakati wa kumbukumbu ya kumuenzi kamanda huyo aliyeuawa miaka minne iliyopita. 

Katika taarifa ya hivi karibuni, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, ameeleza kuwa ziara ya Blinken itaanza leo Alhamisi jioni na atatembelea "miji kadhaa mikuu" ikiwemo pia Israel.

Pia mwanadiplomasia Amos Hochstein atakuwemo kwenye ziara hiyo ya Israel ili kujaribu kuutafutia suluhu mzozo unaonukia kati ya kundi la Hezbollah nchini Lebanon na Israel. Hochstein anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi, Yoav Gallant.

Soma pia: Mapigano yachacha Gaza huku hofu ikizidi juu ya kusambaa kwa vita 

Ziara ya Blinken na Hochstein inalenga kupunguza mvutano kati ya Israel na Hezbollah baada ya kuuawa kwa naibu kiongozi wa Hamas, Saleh Arouri nchini Lebanon.

Naibu kiongozi huyo wa Hamas aliuawa katika shambulio la bomu lililotokea katika kitongoji cha Beirut mnamo siku ya Jumanne na siku moja tu baada ya kifo chake, takriban watu 95 waliuawa kufuatia milipuko miwili iliyotokea karibu na kaburi la jenerali wa jeshi la ulinzi la Iran, Qassem Soleimani katika kumbukumbu ya miaka minne ya kuuawa kwake.

Iran yaapa kuwaadhibu waliohusika na shambulio katika hafla ya kumuenzi Qassem Soleimani

Mji wa Kerman, Iran | Milipuko Iran
Athari za baada ya milipuko miwili kutokea huko Kerman, Iran ambapo takriban watu 95 waliuawaPicha: Tasnim News Agency/AP/picture alliance

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amewanyooshea kidole cha lawama wale aliowaita "wahalifu na maadui waovu wa Iran," na kuongeza kuwa "maafa hayo yatajibiwa vikali, Mungu akipenda."

Naye Rais wa Iran, Ibrahim Raisi ameapa kuwaadhibu wote waliohusika na shambulio hilo, "Nauonya utawala wa Kizayuni: bila shaka kwa shambulio hili na uhalifu mwingine muliofanya, kuwa mutalipa gharama kubwa itakayowafanya mjute."

Soma pia: Zaidi ya watu 100 wameuwawa katika mlipuko Iran 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Matthew Miller ameweka wazi kwamba haikuwa kwa manufaa ya nchi yoyote ile "kuona mzozo huo unatanuka na kuwa mkubwa zaidi ya jinsi ulivyo sasa."

Wakati hayo yanaarifiwa, kundi la Hezbollah na jeshi la Israel, wametoa taarifa kuashiria kwamba mahasimu hao wa muda mrefu wanataka kuepusha kutanuka kwa mzozo kando na mipaka ya Ukanda wa Gaza.

Katika hotuba iliyotolewa jana mjini Beirut, kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliapa kuwa wanamgambo hao wanaoungwa na Iran "hawawezi kunyamaza" kufuatia kifo cha naibu kiongozi wa Hamas Saleh Arouri. Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Magharibi zimeiorodhesha Hamas kama kundi la kigaidi.

Nasrallah amesema vikosi vyake vitapambana hadi mwisho iwapo tu Israel itaamua kuvipeleka vita mlangoni mwa Lebanon, japo hakutoa kitisho cha moja kwa moja kwa Israel.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu hotuba iliyotolewa na kiongozi wa Hezbollah, msemaji wa Ikulu ya Marekani John Kirby aliwaambia waandishi wa habari, "Hatujaoiona Hezbollah ikiitumbukiza miguu yote miwili kwa ajili ya kuisaidia Hamas."