Blinken akutana na rais Abdel Fattah el-Sissi
26 Mei 2021
Blinken aliwasili nchini Misri siku ya Jumatano siku moja baada ya kufanya mazungumzo ya kina na viongozi wa Israeli na Palestina.
Blinken alikutana na rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi na viongozi wengine wakuu serikalini. Blinken ameahidi kushinikiza usaidizi wa kimataifa kujenga upya eneo la ukanda wa Gaza lililoharibika kutokana na mashambulizi ya Israeli huku akiahidi kuhakikisha kuwa hakuna msaada unaotolewa kwa ajili ya eneo hilo unalifikia kundi la Hamas. Badala yake, amesema kuwa wanajaribu kuimarisha mamlaka ya Palsetina inayotambulika kimataifa.
Blinken ameitaja Misri na Jordan kama wadau muhimu katika kujaribu kuleta utulivu katika kanda hiyo. Mataifa yote mawili ni washirika muhimu wa Marekani yaliyo na mikataba ya amani na Israeli na mara kwa mara hutumika kama wapatanishi kati ya Israeli na Palestina.
Hatua iliyochukuliwa na Misri
Misri imetuma ujumbe wake nchini Israeli na katika ukanda wa Gaza kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na pia imekuwa ikisimamia misaada ya kimataifa na msaada wa kujenga upya kwa eneo hilo la Palestina ambalo limekaliwa na Israeli kwa takriban miaka 15.
Blinken amesema leo kuwa Marekani iko katika harakati ya kutoa msaada zaidi wa dola milioni 360 za msaada kwa watu wa Palestina. Hii inajumuisha dola milioni 250 katika maendeleo ya kiuchumi, ulinzi, na msaada wa kiutu uliotangazwa katika miezi ya Machi na Aprili.
Mbali na hayo, serikali ya nchi hiyo inanuia kutoa dola milioni 75 zaidi kuwasaidia Wapalestina pamoja na dola milioni 5.5 kwa usaidizi wa dharura wa kushughulikia majanga katika ukanda wa Gaza pamoja na dola milioni 33 kwa ombi la dharura la
msaada wa kiutu lililotolewa na shirika la wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa. Wiki iliyopita, Sissi aliahidi dola milioni 500 kusaidia katika juhudi za kujenga upya ukanda wa Gaza.