1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter hahofu kukamatwa

31 Mei 2015

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA Sepp Blatter aliechaguliwa tena hahofu kukamatwa kwa uchunguzi wa rushwa wa Marekani dhidi ya maafisa wa soka na ailaumu UEFA kwa kutokuwa na uadilifu kwa wajumbe wa FIFA.

https://p.dw.com/p/1FZVi
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA Sepp Blatter mjini Zurich. (30.05.2015)
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA Sepp Blatter mjini Zurich. (30.05.2015)Picha: Reuters/A. Wiegmann

Baada ya kuchaguliwa kwa muhula mwengine wa miaka mitano na kurudi katika makao makuu ya kifahari ya FIFA mjini Zurich kwa ajili ya mkutano wa kamati kuu na mkutano na waandishi wa habari Jumamosi (30.05.2015) Blatter ameendelea kutamba wakati alipokuwa akijibu masuali ya waandishi wa habari wa kimataifa waliojitokeza kwa wingi.

Blatter amesisitiza kwamba kukamatwa kwa maafisa saba wa FIFA hapo Jumatano siku mbili kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa shirikisho hilo la soka la kimataifa na uchaguzi wake wa rais hakukutokea kwa sadfa lakini hawaogopi maafisa wa serikali ya Marekani walioendesha uchungzi huo.

FIFA ilitingishwa na kufunguliwa mashtaka kwa watu 14 wakiwemo maafisa waandamizi wa FIFA kwa madai ya rushwa na ulaghai yaliyotolewa na maafisa wa serikali ya Marekani.

Hadi sasa saba kati yao wamekamatwa nchini Uswisi na mmoja Trinidad na Tobago. Mbali na hao waliokamatwa kwa ajili ya kujibu mashtaka washtakiwa wengine wanne wamekiri kuwa na hatia kwa madai ya Marekani kuhusiana na rushwa katika FIFA.

Sina wasi wasi

Uchunguzi huo unajumuisha uhamishaji rasmi uliofanywa na FIFA wa dola milioni 10 kwenda kwenye akaunti ya afisa mwandamizi wa zamani wa shirika hilo aliyeingia fedhehani Jack Warner wakati wa kipindi pale Afrika Kusini ilipochaguliwa kuandaa michuano ya soka Kombe la Dunia mwaka 2010 lakini Blatter amesema hakuwa yeye.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA Sepp Blatter mjini Zurich. (30.05.2015)
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA Sepp Blatter mjini Zurich. (30.05.2015)Picha: Reuters/A. Wiegmann

Blatter amekaririwa akiuliza " Kukamatwa kwa ajili gani ?....... Tuache uchunguzi uendelee... kwa hakika mtu huyo sio mimi. Sina dola milioni 10."

Amesema "Iwapo mtu anachunguza wana haki ya kufanya hivyo iwapo watafanya hivyo kwa njia sahihi.Sina wasi wasi na hilo na sina wasi wasi na mimi mwenyewe binafsi."

Blatter amesisitiza kwamba uchunguzi huo hauathiri FIFA moja kwa moja kwa sababu unawahusu "watu binafsi" na FIFA imeathirika "kwa sababu watu hao walikuwa na nyadhifa za kazi FIFA." kama vile makamo wa rais wa FIFA Jeffrey Webb ambaye ni miongoni mwa hao waliokamatwa.

Uadilifu na wema

Mswisi huyo mwenye umri wa miaka 79 kwa kiasi fulani analilaumu shirika la sola la Ulaya kwa kupinga mabadiliko kama vile ya kutaka wajumbe wa kamati kuu ya FIFA wawe wanachaguliwa na Mkutano mkuu wa FIFA baada ya kuchaguliwa na mashirikisho ya soka ambayo yumkini yakawa hayana viwango vya maadli sawa na vile vya FIFA.

Mkutano Mkuu wa FIFA Zurich (29.05.2015)
Mkutano Mkuu wa FIFA Zurich (29.05.2015)Picha: picture-alliance/epa/P. Krämer

Amesema kile tu anachoweza kusema ni kwamba kila mtu anawajibika binafsi kwa maadili yake na matendo yake mema na hawezi kuwafanyia hayo wengine akiwa kama rais wa FIFA.

Ulaya imekuwa ikihitilafiana na Blatter tokea alipoamuwa kuwania tena urais na shirikisho la sola la Ulaya UEFA lililomuunga mkono mpinzani wake Mwana Falme Ali Bin Al Hussein na hasa baada ya matukio ya Jumatano ambapo pia kumeshuhudiwa kuanza kwa uchunguzi rasmi wa Uswisi juu kuchaguliwa kwa Urusi kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na Qatar kuandaa yale ya mwaka 2022.

UEFA lawamani

Blatter ameuambia mtandao wa televisheni ya Uswisi RTS katika mahojiano ya Ijumaa usiku kwamba UEFA na rais wake Michel Platini wamekuwa dhidi yake tokea alipomshinda aliekuwa rais wa wakati huo wa UEFA Lennart Johanson katika uchaguzi wa rais wa FIFA hapo mwaka 1998.

Rais wa shirikisho la soka la Ulaya UEFA Michel Platini.
Rais wa shirikisho la soka la Ulaya UEFA Michel Platini.Picha: Reuters/R. Sprich

Blatter amezungumzia chuki ambayo haitoki kwa mtu mmoja pekee huko UEFA bali katika shirikisho hilo zima ambalo halikufahamu kwamba amechaguliwa kuwa rais hapo mwaka 1998.

Platini alimhimiza Blatter ajiuzulu hapo Alhamisi na Blatter amedokeza kwamba hilo na kukamatwa kwa maafisa wa FIFA sio jambo la sadfa na pia ameona kuna uhusiano kati ya Marekani na Jordan nchi alikozaliwa Mwana Mfalme Ali.

Marekani yakosolewa

Amesema Wamarekani walikuwa wakitaka kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 lakini hawakufanikiwa na kwamba inapasa mtu asisahau kwamba Marekani ni wafadhili wakuu wa nchi ya Kifalme ya Jordan ya mpinzani wake.

Mwana mfalme Ali bin Al Hussein wakati wa mkutano mkuu wa FIFA Zurich. (29.05.2015)
Mwana mfalme Ali bin Al Hussein wakati wa mkutano mkuu wa FIFA Zurich. (29.05.2015)Picha: AFP/Getty Images/F. Coffrini

Amesema hali hiyo haileti ishara nzuri na kuonya kwamba anamsamehe kila mtu lakini hatosahau.

Kamati ya Kuu ya FIFA imeamuwa michuano ya Kombe la Dunia iendelee kuandaliwa na Urusi hapo mwaka 2018 na Qatar iendelee kuandaa ile ya mwaka 2022.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters/AFP/AP

Mhariri : Bruce Amani