1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter auelekea tena urais wa FIFA

1 Juni 2011

Joseph Blatter anaonyesha kuelekea katika muhula wake wa nne na wa mwisho kama Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) katika wakati ambao Shirikisho hilo linakabiliwa na tuhuma kubwa za ufisadi na rushwa.

https://p.dw.com/p/11S8D
Mohamed Bin Hammam (kushoto) na Joseph Blatter
Mohamed Bin Hammam (kushoto) na Joseph BlatterPicha: picture alliance / dpa

Akiwa na umri wa miaka 75, Joseph Blatter anatazamiwa kuchaguliwa tena leo (01.06.2011) mchana, akisalia kuwa mgombea pekee wa wadhifa wa rais wa FIFA.

Kishindo chengine kikubwa kinacholitikisa Shirikisho hilo kinatokea Ujerumani, ambako Shirikisho la Soka la nchi hiyo (DFB) linataka uchunguzi wa jinsi Qatar ilivyopatiwa nafasi ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022.

"Tunajua sote kwamba jahazi ya FIFA inapita katika bahari iliyochafuka, mawimbi makali, lakini lazima tuirekebishe jahazi. Mimi ndiye nahodha, kwa hivyo ni jukumu langu kuirekebisha. Lakini nitafanikiwa tu nikipata msaada wenu nyote - mashirikisho 208 ya FIFA mliofika hapa. FIFA ni shirikisho lenu." Amesema Blatter katika hotuba yake hii leo mjini Zurich.

Makamo Rais wa FIFA, Jack Warner
Makamo Rais wa FIFA, Jack WarnerPicha: picture alliance/dpa

Blatter amependekeza kubadilisha utaratibu wa kuchaguliwa nchi itakayoandaa michuano ya fainali za Kombe la Dunia. Ameshauri jukumu hilo likabidhiwe mkutano mkuu unaohudhuiriwa na wanachama wote na sio kamati kuu tu.

Zaidi ya mashirikisho 170 yanasemekana yameamua kura ipigwe kumchagua raisi wa FIFA huku mashirikisho 17 tu yakipinga.

Dhana kwamba Qatar imependelewa ilipokabidhiwa jukumu la kuandaa michuano ya fainali ya Kombe la Dunia ya mwaka 2022, inaitia sumu FIFA. Mwenyekiti wa DFP, Theo Zwanziger, amesema kuwa anaunga mkono fikra ya kuchunguzwa jinsi Qatar ilivyopatiwa nafasi hiyo.

"Kutokana na yote niliyoyasikia na yote niliyoyasoma katika siku za hivi karibuni, inabidi niseme kutokana na dhana namna zilivyo, watu hawawezi kuziweka kando tu. Ndio maana kuna haja ya kufanyiwa uchunguzi." Amesema Zwanziger katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Ujerumani, ZDF.

Nembo ya FIFA
Nembo ya FIFA

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka la Asia, Mohammed bin Hammam, hajafanikiwa kukata rufaa dhidi ya kuzuiliwa uanachama wake ndani ya kamati kuu ya FIFA. Ametuma malalamiko rasmi kwa FIFA na anasema anafikiria uwezekano wa kutuma malalamiko mbele ya mahakama ya Shirikisho hilo.

Kamati ya Maadili ya FIFA imewafungia Bin Hammam na Makamo Rais wa FIFA, Jack Warner wa Trinidad, kwa kutoa hongo ya dala 40,000 ili kununua kura za mashirikisho ya kitaifa kwa masilahi ya Qatar.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman