Rais wa FIFA asema hapaswi kulaumiwa
10 Julai 2015Mswisi huyo mwenye umri wa miaka 79 hivi karibuni alitangaza kile kilichofasiriwa kuwa kujiuzulu kwake mnamo Juni 2 na FIFA inatarajiwa kuandaa mkutano wa Kamati Kuu mnamo Julai 20 ambao utaweka ratiba itakayotumika kuamua nani atakayeliongoza shirikisho hilo.
Duru za karibu na Blatter zinasema hajafuta uwezekano wa kuubatilisha uamuzi wake wa kujiuzulu. Blatter ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka wa 1998, ameandika katika jarida la kila wiki la FIFA kuwa kuna mada moja tu inayozungumziwa barani Ulaya, ambayo ni uchaguzi wa rais.
Hata hivyo, mageuzi ambayo hayajatekelezwa ndiyo muhimu zaidi. Alisema Blatter. Amesema hilo linastahili nia ya wazi kutoka upande wa Kamati Kuu na Baraza Kuu la FIFA. Blatter amesema hasira ya umma iliyoelekezwa kwa FIFA katika wiki za karibuni imeleekezwa kwake binafsi. Lakini hana tatizo na hilo kwa sababu anaweza kujitetea.
Rais huyo wa FIFA hata hivyo ameomba usawa katika suala hilo maana hawajibiki kwa niaba ya Kamati Kuu ya FIFA kwa sababu hakujichagua mwenyewe.
Fifa siku ya Alhamisi ilimpiga marufuku mwanachama wake wa zamani Chuck Blazer kutoshiriki katika maswala yoyote yanayohusiana na kandanda. Blazer mwenye umri wa miaka 70 alifanya kazi kama mpelelezi na maafisa wa mashtaka nchini Marekani baada ya kukiri kuhusika na mashtaka ya kutoa hongo na ukwepaji wa kodi.
Mnamo mwezi Mei, maafisa saba wa FIFA walikamatwa kwa mashtaka ya udanganyifu wa kutaka kupata fedha. Mamlaka za Uswisi zimesema mmoja wa maafisa hao amekubali kusafirishwa nchini Marekani ili kujibu mashtaka yanayomkabili
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman