Bingwa La Liga kujulikana dakika ya mwisho
18 Mei 2017Real Madrid inahitaji alama moja pekeyake kunyakua ubingwa wa taji hilo ambalo limewakwepa tangu mwaka 2012, ingawa itakuwa inakabiliana na Malaga ambayo imekuwa na mchezo wa kuridhisha katika mechi zake za hivi karibuni.
Ikiwa katika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi hiyo, Malaga imeshinda mechi nne mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani La Rosaleda, ambapo wamewadunga Barcelona, Valencia, Sevilla na Celta Vigo.
Matumaini ya Barcelona kulinyakua taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo yanategemea iwapo wataibwaga Eibar na Madrid wapoteze mchuano wao.
Nafasi mbili zilizosalia za kushiriki ligi ya vilabu bingwa msimu ujao zimeshikiliwa na Atletico Madrid na Sevilla walio katika nafasi ya nne, na kutokana na hilo Sevilla watashiriki mechi za mtoano mwezi Agosti ili wafuzu kwenye hatua ya makundi ya ligi hiyo ya mabingwa.
Nafasi mbili za kushiriki ligi ya Ulaya msimu ujao katika ligi hiyo zinashikiliwa na Villareal na Athletic Bilbao ingawa Real Sociedad bado wana nafasi pia. Villareal walio na alama moja pekeyake mbele ya Bilbao watakuwa wanakwaana na Valencia katika ngarambe yao ya mwisho, nao Bilbao wasafiri kuelekea Madrid kujaribu bahati kwa Atletico Madrid.
Sociedad wao watapambana na Celta Vigo katika mechi ya mwisho na wako chini ya Atlhletic Bilbao katika jedwali kutokana na rekodi yake hafifu ya ushindi walipokutana na hao Bilbao.
Granada, Osasuna na Sporting Gijon ndizo timu ambazo tayari zishashushwa daraja katika La Liga.
Mwandishi: Jacob Safari/APE
Mhariri: Bruce Amani