1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, viongozi wa dunia waihimiza Hamas kukubali mpango

6 Juni 2024

Rais Joe Biden wa Marekani na viongozi wengine 16 wa dunia kwa pamoja wamelihimiza kundi la Hamas kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/4gkII
Mapigano Gaza
Mashambulizi yanaendelea kushuhudiwa katika Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa Picha: Ali Jadallah/AA/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House imesema viongozi hao wameziambia pande hasimu kwamba hakuna wakati wa kupoteza na kuitolea mwito Hamas kukubali pendekezo la usitishwaji vita.

Taarifa hiyo ilitiwa saini na viongozi wa mataifa makuu ya Ulaya yakiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Uhispania, ambayo imeikasirisha Israel kwa kulitambua taifa la Palestina.

Katika hali isiyo ya kawaida zaidi, kauli hiyo iliwaleta pamoja viongozi waliotofautiana kiitikadi wa mataifa ya Amerika Kusini: Brazil na Colombia, ambayo marais wake wameikashifu Israel, na Argentina, ambayo kiongozi wake mpya anaiunga mkono Israel.

Biden wiki iliyopita alitangaza hadharani mpango mpya ambao unapendekeza Israel kujiondoa kutoka kwa maeneo yenye watu wengi huko Gaza na Hamas kuwaachilia mateka.