1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akosolewa jinsi anavyoshughulikia mripuko wa COVID-19

16 Machi 2020

Makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Joe Biden na Seneta wa Vermont, Bernie Sanders jana wameshiriki katika mdahalo wa ana kwa ana kwa ni mara ya kwanza.

https://p.dw.com/p/3ZV4Q
Präsidentschaftskandidaten Bernie Sanders und Joe Biden
Picha: Reuters/J. Ernst

Makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Joe Biden na Seneta wa Vermont, Bernie Sanders jana wameshiriki katika mdahalo wa ana kwa ana kwa ni mara ya kwanza.

Biden na Sanders wanaowania kuchaguliwa katika kura za mchujo za kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic wamekutana katika mdahalo wa 11 ambao ulihamishwa kutoka Arizona, kutokana na hofu ya kuenea kwa virusi vya corona na ambao ulifanyika bila ya kuwa na watazamaji.

Baada ya kukutana katika ukumbi unakofanyika mdahalo huo mjini Washington, wagombea hao wawili walisalimiana kwa kugonganisha kiwiko. Biden ameahidi kumteua mwanamke kuwa mgombea mwenza, iwapo atashinda kuwania kinyang'anyiro hicho kupitia chama cha Democratic.

''Iwapo nitachaguliwa kuwa rais, ninaahidi nitamteua mwanamke kuwa makamu wa rais. Kuna wanawake kadhaa ambao wana sifa ya kuwa marais kesho. Nitamchagua mwanamke kuwa makamu wangu,'' alisisitiza Biden.

Biden arejea ahadi ya mwezi uliopita

Pia Biden amerejea ahadi yake aliyoitoa katika madahalo wa mwezi uliopita kwamba atamteua mwanamke mweusi kuwa Jaji katika Mahakama ya Juu ya Marekani. Kinyang'anyiro cha nafasi za mchujo kuwania urais kwa chama cha Democratic kimegeuka kuwa mashindano ya watu wawili kati ya Biden na Sanders ambao wote umri wao ni kwenye miaka ya 70.

Kwa upande wake Sanders amesema bila shaka kuna uwezekano pia akamteua mwanamke. ''Kwangu mimi sio tu kumteua mwanamke, bali kuhakikisha kwamba tuna mwanamke anayeunga mkono mageuzi ya kijamii na kutaka maendeleo. Kuna wanawake wengi wa aina hiyo. Hivyo nia yangu ni kwenda katika mwelekeo huo,'' alifafanua Sanders.

US-Präsident Trump spricht über die Reaktion der USA auf die COVID-19-Coronavirus-Pandemie
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Reuters/D. Mills

Sanders amesema mfumo wa sasa wa afya nchini Marekani, ambako watu wengi wako kwenye mashirika binafsi ya bima ya afya unaolipiwa na waajiri wao, ni wa gharama kubwa na usiofaa, hivyo kuwaacha maelfu ya watu kila mwaka wakiugua magonjwa yanayoweza kuzuilika. Amesema virusi vya corona vimezidi kuyafanya mambo kuwa mabaya zaidi.

Wakati huo huo, wagombea hao wawili wamemkosoa Rais Trump kutokana na anavyolishughulikia janga la COVID-19. Sanders amesema iwapo angekuwa rais, angehakikisha kwamba hakuna mtu anayelipia huduma ya kupima virusi hivyo. Kwa upande wake Biden amesema pia anaamini kwamba hakuna mtu anayepaswa kulipia huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Biden, kila jimbo linahitaji kuwa na angalau maeneo 10 ya kupima virusi vya corona na wizara ya ulinzi pamoja na idara ya dharura ya shirikisho zinahitaji kuratibu mipango ya kuongeza vitanda vya hospitali.

Kuenea kwa kasi virusi hivyo kumesababisha wagombea hao kuahirisha mikutano kadhaa ya kampeni zao, hata wakati ambapo baadhi ya majimbo makubwa kama vile Illinois, Ohio, Florida na Arizona yanajiandaa kupiga kura siku ya Jumanne.

Wagombea hao wamezungumzia pia masuala ya kiuchumi, sera ya kigeni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, huku Sanders akimshutumu Biden kwa kutoonyesha mipango ya kutosha katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

(AP, Reuters, DW)