Biden: Mustakabali wa Ireland Kaskazini ni wa Marekani pia
12 Aprili 2023Akizungumza Jumatano katika Chuo Kikuu cha Ulster mjini Belfast, wakati nchi hiyo ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 ya Mkataba wa kuleta amani maarufu kama Ijumaa Kuu, Biden amesema makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Marekani yalileta amani katika sehemu hiyo ya Uingereza, lakini mzozo mpya wa kisiasa hivi karibuni umeitikisa nguvu yake. Biden amesema nchi hiyo haitorejea nyuma katika enzi za machafuko.
''Ukweli ni kwamba amani na fursa ya kiuchumi zinakwenda sambamba. Katika miaka 25 ya Makubaliano ya Ijumaa Kuu, pato la ndani la Ireland Kaskazini limeongezeka maradufu. Kuna mashirika mengi makubwa ya Kimarekani yanayotaka kuja hapa kuwekeza,'' alifafanua Biden.
Uwekezaji wa Marekani kusaidia ukuaji wa uchumi
Katika ziara yake ya kwanza kama rais Ireland Kaskazini, Biden amesisitiza kwamba uwekezaji wa Marekani unaweza kusaidia kuchochoea ukuaji wa uchumi, hasa iwapo wanasiasa wenye mifarakano huko Belfast, watatatua tofauti zao za kisiasa ambazo zimesababisha mkwamo wa serikali. Biden amesema historia ya Ireland Kaskazini ni historia ya Marekani, na muhimu zaidi mustakabali wa Ireland Kaskazini pia ni mustakabali wa Marekani.
Katika hotuba yake, Biden aliwamwagia pongezi watu waliokuwa tayari kuonesha ujasiri wao kwa ajili ya siku zijazo, kwa kufikia makubaliano, huku akiikumbusha hadhira kuwa suala la amani lilikuwa haliepukiki. Amesema ingawa amani hiyo imedumu, Ireland Kaskazini kwa sasa haina serikali inayofanya kazi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak amesema uhusiano kati ya Uingereza na Marekani uko katika hali nzuri. Akizungumza muda mfupi baada ya kukutana Jumatano asubuhi kwa chai pamoja na Biden, Sunak amesema wamejadiliana kuhusu fursa za kiuchumi katika eneo hilo ambalo ni sehemu ya Uingereza.
''Sisi ni washirika wa karibu sana, tumezungumza mambo mbalimbali. Tumezungumza hasa kuhusu fursa za kiuchumi zilizoko Ireland Kaskazini, na pia uwezekano wa uwekezaji uliopo, na kampuni zinazotaka kuwekeza Ireland Kaskazini,'' alisema Sunak.
Kiongozi wa DUP: Ziara ya Biden kutobadili siasa za Ireland Kaskazini
Biden amekutana pia na viongozi wa vyama vitano vikuu vya siasa vya Ireland Kaskazini, katika Chuo Kikuu, kabla ya kuhutubia. Hata hivyo, kiongozi wa Chama cha Democratic Unionist, DUP Jeffrey Donaldson amesema ziara ya Biden Ireland Kaskazini, haitobadilisha mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo, wala kubadili msimamo wa chama chake kuisusia serikali ya eneo hilo ya kugawana madaraka.
Akizungumza baada ya kukutana na Biden, Donaldson amewaambia waandishi habari kwamba wanajua wanachohitaji kifanyike, ambacho ni serikali ya Uingereza kwenda mbali zaidi katika kuilinda nafasi ya Ireland Kaskazini ndani ya Uingereza na kuonesha uwezo wao wa kufanya biashara ndani ya soko la Uingereza.
(DPA, AFP, AP, Reuters)