1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kushiriki mkutano wa NATO mataifa ya Ulaya Mashariki

10 Mei 2021

Rais wa Marekani Joe Biden ataungana katika mkutano kwa njia ya vido na marais wa mataifa yalioko kwenye upande wa mashariki ya jumuiya ya kujihami NATO, unaofanyika Jumatatu katika mji mkuu wa Romania.

https://p.dw.com/p/3tCwG
Litauen NATO-Truppen
Picha: Getty Images/AFP/P. Malukas

Mengi ya mataifa hayo yana wasiwasi unaofanana kuhusu majaribio ya Urusi kurejesha ushawishi wake katika kanda hiyo, na wasiwasi huo umeongezeka zaidi baada ya Urusi kuitwaa kwa nguvu rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014.

Rais wa Romania Klaus Iohannis, mwenyeji wa mkutano huo, alisema kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter, kwamba anafurahi kumkaribisha Biden, na kuwa mkutano huo ni maandalizi ya mkutano kamili ya jumuiya ya NATO wa mwezi ujao.

Soma pia: Nato wajadili mageuzi

Amesema mkutano wa leo, ulioandaliwa kwa pamoja na rais Poland Andrzej Duda, utajumlisha mazungumzo ya ulinzi na uzuwiaji kwenye upande wa mashariki wa muungano wa NATO, na kwamba katibu mkuu wa jumuiya hiyo Jens Stoltenberg anashiriki pia.

Duda alisema wakati wa mkutano wa habari kabla ya mkutano huo kwamba Ukraine pia itakuwa kwenye ajenda ya mazungumzo.

Belgien NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg.Picha: John Thys/AP/picture alliance

Alisema amepata ahueni kwamba Urusi ilirudisha nyuma sehemu kubwa ya majeshi yake ambayo ilikuwa imeyarundika hivi karibuni karibu na mpaka wa Ukraine, akisema anaamini hilo lilipunguza hatari ya uvamizi mwingine wa Urusi.

Lakini akaongeza kuwa hakuna mashaka kwamba hali katika eneo la mashariki mwa Ukraine ni ngumu, na kwamba ardhi ya Ukraine inakaliwa kimabavu.

"Si Ulaya wala dunia inayoweza kuondoa nadhari yake kwenye sehemu hii ya bara letu", alisema Duda, na kuongeza kuwa "sote tunapaswa kuiunga mkono Ukraine, lakini wakati huo huo tuchukue hatua kulinda usalama wetu."

Kundi la Bucharest Tisa

Wanachama wa kundi la Bucharest Tisa ni Romania, Poland, Hungary, Bulgaria, Jamhuri ya Czech, Slovakia, pamoja na mataifa matatu madogo ya Baltic, Estonia, Latvia na Lithuania.

Soma pia: NATO, EU wamwalika Biden kujenga upya uhusiano na Marekani

Mataifa hayo yote yalikuwa yanadhibitiwa na Moscow wakati wa Vita Baridi, ambapo mataifa ya Baltic yalikuwa yamejumuishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti. Hivi sasa yote ni wanachama wa Umoja wa Ulaya na NATO, na  muungano huo wa kijeshi umeongeza uwepo wake katika kanda baada ya Urusi kuivamia Ukraine.

Belgien Brüssel | Rumänischer Präsident | Klaus Iohannis
Rais wa Romania Klaus Iohannis.Picha: Getty Images/AFP/A. Oikonomou

Siku ya Jumanne, Iohannis na Duda watahudhuria mazoezi ya kijeshi yanayoyahusisha majeshi ya Romania na Poland, yanayoitwa "Justice Sword 21", katika eneo la Smardan, mashariki mwa Romania.

Mkutano huo wa mataifa tisa ya kati na mashariki mwa Ulaya unakuja kabla ya mkutano wa kilele wa NATO Juni 14 mjini Brussels, ambako muungano huo una makao yake makuu.

Kwenye mkutano huo wa kilele, Biden na viongozi wengine wanapanga kujadili uhusiano tete na Urusi na China, kuondolewa kwa vikosi kutoka Afghanistan na mustakabali wa muungano huo wenye mataifa wanachama 30.

Chanzo: AP