1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kuapishwa rais wa 46 wa Marekani

20 Januari 2021

Mdemokrat Joe Biden ataapishwa leo kuwa rais wa 46 wa Marekani. Biden atachukua usukani katika nchi ambayo imezongwa na migawanyiko mikubwa ya kisiasa na ambayo inaendelea kuathiriwa zaidi na janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3o9us
Designierter Präsident der USA Joe Biden
Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance

Biden mwenye umri wa miaka 78 atakuwa rais wa Marekani mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya taifa hilo.

Biden atakula kiapo cha urais mbele ya jaji mkuu wa Marekani John Roberts adhuhuri majira ya taifa hilo, akishika bibilia ambayo familia ya Biden imekuwa ikimiliki kwa zaidi ya nusu karne.

Hata hivyo hafla ya kuapishwa kwake itahudhuriwa na idadi ndogo ya watu, yaani waalikwa pekee. Sherehe hiyo mjini Washington haitakuwa na shamrashamra kama za watangulizi wake kufuatia janga la COVID-19 na pia kutokana na hofu za kiusalama baada ya kisa cha wafuasi wa rais anayeondoka Donald Trump kuvamia majengo ya bunge Capitol Hill mjini Washington Januari 6.

Takriban bendera 200,000 katika eneo atakapoapishwa Biden kuashiria Wamarekani.
Takriban bendera 200,000 katika eneo atakapoapishwa Biden kuashiria Wamarekani.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Usalama waimarishwa

Maelfu ya wanajeshi kutoka kikosi cha ulinzi wa taifa nchini humo wamepelekwa katika mji mkuu Washington kushika doria na vilevile katika miji mingine kufuatia tahadhari iliyotolewa na idara ya upelelezi ya Marekani FBI kuwa kuna mipango ya watu wenye silaha kuandamana wakati wa kuapishwa kwa Biden.

Soma pia: 

"Tunaenda kushirikiana na kikosi cha ulinzi wa rais  pamoja na FBI na wengine kuhakikisha tunafanya kila tuwezalo na tukishirikiana kila upande ili rais mteule na makamu wa rais mteule wako waapishwe kwa njia salama." Amesema Jonathan Hoffman ambaye ni msemaji mkuu wa Pentagon.

Badala ya umati mkubwa wa wafuasi wa Biden kuhudhuria, kutakuwa na takriban bendera 200,000 na minara 56 ya taa kuashiria Wamarekani, majimbo na mamlaka mbalimbali nchini humo.

Baadhi ya wanajeshi wa ulinzi wa taifa ambao wamepelekwa kuimarisha usalama Washington katika hafla ya kuapishwa kwa Biden.
Baadhi ya wanajeshi wa ulinzi wa taifa ambao wamepelekwa kuimarisha usalama Washington katika hafla ya kuapishwa kwa Biden.Picha: Rebecca Blackwell/AP Photo/picture alliance

Sherehe hiyo itafanywa chini ya usalama wa hali ya juu, mahali ambapo wafuasi wa Donald Trump walivamia majengo ya bunge wiki mbili zilizopita, kufuatia ghadhabu zao wakidai uchaguzi ambao Biden alishinda ulikumbwa na udanganyifu. Watu watano walifariki kufuatia vurugu hizo.

Kufuatia uvamizi huo baraza la wawakilishi linalodhibitiwa na Wademokrat nchini Marekani lilipitisha kwa mara ya pili mashtaka ya kumvua madaraka DonaldTrump wiki iliyopita.

Trump kutohudhuria hafla ya kumuapisha Biden

Aliyekuwa mgombea mwenza wa Biden, Kamala Harris ambaye ni mzaliwa wa familia ya walokuwa wahamiaji kutoka Jamaica na India, atakuwa mwanamke wa kwanza na pia ambaye asili yake ni mchanganyiko wa Asia na Amerika kuwa makamu wa rais punde tu atakapoapishwa na jaji wa mahakama ya juu Sonia Sotomayor kuhudumu kwenye wadhifa huo.

Rais anayeondoka madarakani nchini Marekani Donald Trump akiwapungia maafisa wake mkono , wakati akiabiri ndege baada ya kutembelea mpaka wa Marekani na Mexico Januari 12, 2021.
Rais anayeondoka madarakani nchini Marekani Donald Trump akiwapungia maafisa wake mkono , wakati akiabiri ndege baada ya kutembelea mpaka wa Marekani na Mexico Januari 12, 2021.Picha: Carlos Barria/REUTERS

Katika hotuba yake ya kuapishwa, Biden ambaye ameapa kurejesha mshikamano wa Marekani, atatoa wito wa umoja mnamo wakati nchi yake inazongwa na mizozo. Hayo ni kulingana na washauri wake.

Rais Trump ambaye hadi sasa hajakubali rasmi kushindwa katika uchaguzi hu owa Novemba 3, amepanga kuondoka ikulu ya Whitehouse kabla ya hafla ya kuapishwa kwa Biden na hatahudhuria. Hatua ambayo ni kinyume na utamaduni wa kisiasa ambao umekuwepo Marekani kwa zaidi ya karne moja na nusu ya kukabidhiana madaraka kwa amani.

Badala yake Trump atakuwa na hafla binafsi ya kuagwa katika uwanja wa ndege wa kijeshi karibu na mji wa Washington.

Obama, Bush na Clinton kuhudhuria hafla

Makamu wa Rais Mike pence pamoja na marais wa zamani wa nchi hiyo George W. Bush, Barack Obama na Bill Clinton ni miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria. Watu wengine maarufu akiwemo mwanamuziki Jennifer Lopez pia watahudhuria.

Katika saa za mwisho mwisho wa utawala wake, Trump amewapa tena msamaha watu 73, akiwemo msaidizi wake wa zamani Steve Bannon. Hayo ni kulingana na taarifa kutoka White House.

(RTRE, AFPE, DPAE)