Biden ayafuta maagizo ya Trump juu ya mazingira na uhamiaji
21 Januari 2021Kwa kuyasaini maagizo hayo Rais Biden amedhamiria kuonyesha mabadiliko makubwa ya mwelekeo wa siasa za Marekani. Mshauri wake kuhusu magonjwa ya miripuko, Dr Anthony Fauci ameuhutubia kwa njia ya video mkutano wa shirika la Afya ulimwenguni WHO, na kuarifu kuwa Marekani inajiunga na ushirika wa kidunia kwa ajili ya chanjo kwa wote.
Soma zaidi: Viongozi duniani wampongeza Biden na Kamala
Aidha, Dr Fauci ameahidi kuwa Marekani itarejea tena katika shirika la WHO kama mwanachama.
''Ninayo fahari kutangaza kuwa Marekani itabakia kuwa mwanachama wa WHO. Jana Rais Joe Biden alisaini barua inayofuta tangazo la kujiondoa katika shirika hilo, na barua hiyo tayari imetumwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kwako Dr Tedros, rafiki yangu.'' Amesema Dr Fauci katika mkutano huo.
Tedros Adhanom Ghebreyesus ni mkurugenzi mkuu wa WHO ambaye mwaka jana alikosolewa vikali ya Donald Trump, kabla ya rais huyo aliyepita wa Marekani kuiondoa nchi yake katika shirika la afya ulimwenguni, alilolituhumu kushindwa vibaya katika mapambano dhidi ya janga la corona. Dr Fauci pia alithibitisha kuwa Marekani inarejesha ufadhili wa kifedha kwa shirika hilo.
Mchaka-mchaka kupambana na COVID-19
Agizo la kujiunga tena na WHO, pamoja na kurejea katika makubaliano ya kimataifa ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa maagizo 17 aliyosaini Biden mnamo siku yake ya kwanza madarakani.
Soma zaidi: Biden kusaini maagizo ya kiutendaji baada ya kuapishwa
Na leo hii rais huyo anatarajiwa kuyasaini mengine 10, yanayohusu moja kwa moja mapambano dhidi ya janga la COVID-19 ambalo limeambukiza Wamarekani zaidi ya milioni 24.5, na kuwauwa wasiopungua 400,000.
Maagizo hayo ya kiutendaji ni pamoja na ulazima wa kuvaa barakoa katika majengo yote ya serikali ya shirikisho, na kutumia sheria ya uzalishaji wa kiulinzi kuwezesha utengenezaji wa vifaa vya kutosha kuwakinga watu dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Dunia yashusha pumzi ya ahueni
Viongozi wengi muhimu duniani wamesifu mwelekeo mpya wa Marekani baada ya Trump kuondoka. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema leo kuwa kwa kuzingatia maagizo aliyoyasaini Biden, ni wazi kuwa wigo wa ushirikiano baina ya Marekani na Ujerumani umepanuka.
Soma zaidi: Biden azindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema vipaumbele vya Rais Joe Biden vinashabihiana na vile vya Uingereza, vikiwemo ulinzi wa mazingira na mapambano dhidi ya virusi vya corona.
China, ambayo ilikabiliwa na mbinyo mkali wa Marekani chini ya uongozi wa rais Donald Trump, imesema kupitia wizara yake ya mambo ya nje, kuwa inatazamia kuboreka kwa mahusiano baina ya mataifa hayo mawili yanayoongoza kiuchumi duniani, na ushirikiano katika kuzishughulikia changamoto zinazoikumba dunia.
Vyanzo: ape, rtre