Biden atangaza muelekeo mpya wa siasa za nje za Marekani
5 Februari 2021Akitangaza kile alichokiita kurejea rasmi kwa Marekani kwenye uwanja wa diplomasia ya kilimwengu, Biden aliwaambia wanadiplomasia kwenye Wizara ya Mambo ya Kigeni ya nchi yake kwamba wana jukumu kubwa la kurekebisha mule mote mulimovurugwa panapohusika taswira ya taifa lake duniani:
"Marekani imerehea. Marekani imerejea. Diplomasia imerejea kwenye kiini cha sera yetu ya mambo ya nje. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu ya kuapishwa, tutarekebisha mahusiano na washirika wetu, na tutajihusisha tena na ulimwengu sio kwa kukabiliana na changamoto za jana, bali za leo na za kesho," alisema kiongozi huyo.
Mahsusi kabisa, Biden alitumia hotuba hiyo kuonesha utayari wa serikali yake kuhakikisha kuwa Marekani inasimama imara mbele ya mahasimu wake wa jadi, Urusi na China, lakini kwa njia ambazo hazitahatarisha mataifa mengine.
Biden alisema Marekani na Urusi zimekubaliana kuongeza muda wa mkataba mpya wa kusitisha mashindano ya silaha kati yao kwa kipindi cha miaka mitano, na hivyo kuulinda mkataba pekee kati ya nchi hizo juu ya nyuklia.
"Nimemwambia wazi Rais Putin kwamba mimi ni tafauti sana na mtangulizi wangu, lakini siku za Marekani kuvivumilia vitendo vya Urusi kuuingilia uchaguzi wetu, mashambulizi ya mitandaoni, kuwapa sumu raia wake, zimekwisha. Hatutasita kuifanya Urusi ilipie gharama za hayo na kuyalinda maslahi na watu wetu," alisisitiza.
Asimamisha uungaji mkono vita vya Yemen
Biden aliyefuatana na makamu wake, Kamala Harris, alitumia hotuba yake hiyo iliyojenga msingi wa siasa za nje za Marekani kwenye utawala wake kutangaza pia kusimamisha uungaji mkono wa nchi yake kwa vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen, akisema hiyo ni hatua mojawapo ya msimamo wa Marekani kuhimiza diplomasia, demokrasia na haki za binaadamu duniani kote.
Rais huyo mpya wa Marekani alisema vita hivyo lazima vikomeshwe mara moja, kwani vimeleta balaa la kibinaadamu na la kimkakati, ingawa alionekana kutokuwa tayari kuiwacha mkono Saudi Arabia, mshirika muhimu wa Marekani kwenye eneo la Ghuba.
"Vita hivi lazima vimalizike, na kuonesha jinsi nilivyodhamiria, tunasitisha msaada wote wa Marekani kwenye operesheni za kijeshi katika vita vya Yemen, yakiwemo mauzo ya silaha. Wakati huo huo, Saudi Arabia inakabiliwa na mashambulizi ya makombora na vitisho vingine kutoka kwa vikosi vinavyopewa silaha na Iran katika nchi kadhaa. Tutaendelea kuisadia Saudi Arabia kulinda mamlaka, mipaka, na watu wake."
Hotuba hiyo ya Biden ilielezea pia msimamo wa Marekani dhidi ya mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar, ambapo alitaka kurejeshwa mara moja kwa utawala wa kiraia.